Mertesacker ataja udhaifu wa Wenger ulivyoipoteza Arsenal

Wednesday September 11 2019

 

LONDON, ENGLAND.PER Mertesacker amesema Arsene Wenger amekuwa na udhaifu mmoja wa kuwaamini sana wachezaji hata kama hawakuwa wakimpatia matokeo mazuri kwenye mechi.

Beki huyo Mjerumani mwenye umri wa miaka 34 kwa sasa, alicheza miaka saba chini ya Mfaransa huyo huko kwenye kikosi cha Arsenal.

Mwishoni mwa msimu uliopita, Wenger alihitimisha miaka yake 22 ya kuitumikia Arsenal, akiondoka hapo na rekodi ya kubeba Ligi Kuu England mara tatu na Kombe la FA mara saba.

Lakini beki Mertesacker anafichua kile kilichokuwa kikimwaangusha Wenger asipate mafanikio makubwa zaidi huko kwenye kikosi cha Arsenal.

Katika kitabu chake, 'Per Mertesacker: Big Friendly German', beki huyo aliandika: "Tulipopoteza mechi, basi tuliendelea kupoteza nyingine mfululizo zilizofuatia. Tungeweza kuonyesha ubora wetu kwenye mechi sita za Kombe la FA, lakini kwenye mechi 38 za Ligi Kuu England za kucheza kwa miezi 10 tulikuwa watu wengine kabisa.

"Tulishindwa kuwa na ule mwendelezo wa ushindi kama timu kubwa. Huwezi kushinda ubingwa wa ligi kama unapoteza mechi nane ndani ya msimu. “Kocha Arsene Wenger siku zote yeye alikuwa mtu wa kuamini timu yake, hakuwahi kukosa matumaini.

Advertisement

"Hakuwahi kukasirika hata kama tunapoteza mfululizo. Alibaki kuwa upande wa watoto wake, hata kama anashinikizwa kiasi gani. Hii ni imani ya hali ya juu. Nadhani ndio uliokuwa udhaifu wake mkubwa.

“Mashabiki walikuwa wakimshambulia, angekuwa anawasikiliza, basi kungekuwa na usajili mpya wa wachezaji wasiopungua watano kila mwaka.

"Majukwaani mashabiki walikuwa wakimtusi wakitaka atumie pesa kusajili kwenye mechi za vipigo, lakini Wenger siku zote aliendelea kuwaamini wachezaji aliokuwa nao. Binafsi sijawahi kukutana na kocha mwingine kama huyo aliyekuwa na imani kubwa kwa wachezaji wake."

Advertisement