Meja Kunta awapagawisha mastaa Ligi Kuu

Saturday May 23 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA THOMAS NG'ITU

MSANII wa muziki wa Singeli, Meja Kunta amegeuka kuwa kivutio katika mazoezi ya wachezaji wa timu mbalimbali za Ligi Kuu ambayo yamekuwa yakifanyika katika fukwe za bahari eneo la Escape One.

 Mbali ya wachezaji wa Ligi Kuu, mazoezi hayo pia hushirikisha wachezaji wa timu za madaraja ya chini yakisimamiwa na kipa wa KMC, Juma Kaseja.

Meja Kunta amekuwa kivutio katika eneo la kwanza ambalo ni kuimba nyimbo zake ambazo zimekuwa zikipigwa katika spika ambayo huletwa na Kaseja ambapo msanii huyo amekuwa akizifuatisha na kutumbuiza, jambo ambalo huwakosha wengi na wengine kujikuta wakizicheza.

Kutokana na kuwakosha wengi, msanii huyo amekuwa akifanya hivyo kabla na baada ya kumaliza programu zao za mazoezi.

Jambo lingine ambalo Meja Kunta amekuwa kivutio uwanjani hapa ni uwezo wake wa kucheza mpira

Kama ikitokea Meja amepiga pasi nzuri, chenga, kisigino au madoido ya aina yoyote ile wachezaji waliokuwa ndani ya uwanja na hata wale wa nje huanza kushangilia na  wengine kumpandia mgongoni kama ishara ya kumpongeza.

Advertisement

Meja anasema anafanya mazoezi hayo ili kuwa fiti na kupata pumzi ambayo itakwenda kumsaidia katika shughuli zake za  kuimba .

 "Kwanza mafurahi kupewa nafasi hii kufanya mazoezi na watu wa Ligi Kuu si kazi rahisi ndio maana nimekuwa nikihimili na kufanya kama wao kwani natambua hapa wapo kazini.

" Kuhusu uwezo ambao naonesha hapa watu kama hawafahaku kabla ya kuanza kuimba ndoto zangu zilikuwa kucheza soka na hata miaka ya nyuma nimepita katika akademi mbalimbali," anasema Meja Kunta.

Msanii huyo amejizolea umaarufu mkubwa katika siku za hivi karibuni kutokana na nyimbo zake za ‘Mamu’ na ‘Wanga Wabaya’.

 

 

Advertisement