Mechi za mchana zinaweza kusababisha kifo kwa wachezaji

Muktasari:

  • Wachezaji wanapocheza wakati wa jua kali wanakuwa katika hali ya kukausha maji mwilini kwa haraka na hivyo kuwepo na hatari ya kupatwa na shambulio la moyo au kuziba moyo misuli kukakamaa

Tanga. Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimeshauriwa kubadilisha uamuzi wao wa kupanga mechi za Ligi Kuu kuchezwa saa 8.00 mchana kwa sababu kitaalamu inaweza kuleta madhara kwa wachezaji ikiwamo kufa uwanjani.

Ushauri huo umetolewa na mtaalamu wa misuli ya mwili wa binadamu Dk Kitambi Mganga baada ya kumalizika kwa mchezo baina ya Simba na Coastal Union ulioanza saa 8.00 kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Dk Mganga alisema wachezaji wanapocheza wakati wa jua kali wanakuwa katika hali ya kukausha maji mwilini kwa haraka na hivyo kuwepo na hatari ya kupatwa na shambulio la moyo au kuziba moyo misuli kukakamaa.

“Shambulio la moyo inatokana na mwili kulazimishwa kufanya kazi ngumu wakati wa jua kali, moyo unaziba, ulimi unatoka nje, misuri inashindwa kufanya kazi ni hatari kubwa mchezaji anaweza kupoteza maisha uwanjani kama hakuta kuwa na mtaalamu mwenye kujua atoe huduma gani,”alisema Dk Mganga.

Mtaalamu huyo ameishauri bodi ya Ligi itafute namna nyingine ya kupanga mechi za ligi kuu badala ya saa 8.00 kwa sababu kuna hatari ya kupoteza maisha ya wachezaji uwanjaini.

Mtaalamu huyo ambaye ni Daktari wa Coastal Union, aliyetumikia nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, alisema kama kuna ulazima wa kchezesha mechi hizo katika muda huo basi mwamuzi anaweza kutenga hata dakika moja ya kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji na inafanyika hivyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Stephen Mguto alisema kuchezeshwa mchana kwa mechi hizo kulitokana na kuipa nafasi michuano ya AFCON inayoendelea jijini Dar es salaam.

“Tunakimbizana na muda, tumepanga mechi hizi mchana kwa sababu ya michuano ya Afcon inayoendelea jijini Dar es salaam,”alisema Mguto.