Mechi hizi kuamua hatma kupanda VPL

Muktasari:

Hatma ya nani atapanda Ligi Kuu kutoka kwenye timu hizo itajulikana baada ya michezo mitano ijayo kwa kila timu kuanzia wikiendi hii hadi ile michezo ya 19 watakayocheza.

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea wikiendi hii katika mzunguko wa 15 kwa timu kutafuta alama tatu zitakazowawezesha kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Dodoma FC ndio inaongoza kundi A, ikiwa na alama 30 ikifutiwa na Ihefu FC yenye alama 27 na Mbeya Kwanza FC ikiwa nafasi ya tatu kwenye kundi hilo na alama zao 25.

Kundi B nako bado mambo yamezidi kuwa mazito kwa Gwambina FC iliyokaa kileleni kwa kukusanya alama 28, huku Geita Gold ikifukuzia nafasi hiyo kwa karibu baada ya kukusanya alama 25 na Arusha FC ikiwa nafasi ya tatu na alama 23.

Hatma ya nani atapanda Ligi Kuu kutoka kwenye timu hizo itajulikana baada ya michezo mitano ijayo kwa kila timu kuanzia wikiendi hii hadi ile michezo ya 19 watakayocheza.

Kinara Dodoma FC inaanza kibarua chake leo Jumamosi mbele ya Ihefu FC kwenye Uwanja wa Highland Estates jijini Mbeya na endapo itashinda mchezo huo itawaacha wapinzani wake alama sita, lakini ikipoteza kazi inaanza upya ya nani watakaa kileleni huku Mbeya Kwanza ikicheza na Majimaji FC inayokamata nafasi ya nne.

Baada ya hapo Ihefu itacheza na Iringa United inayoburuza mkia wa kundi hilo na Dodoma FC itacheza na Pan African ambayo nayo ipo nafasi ya pili kutoka mkiani, hivyo kila timu inasaka alama tatu na Mbeya Kwanza ikicheza na Boma ambayo bado ipo kwenye msafara wa kusaka nafasi ya kwenda VPL.

Mchezo wa 17 utakuwa na dabi ya Mbeya Kwanza dhidi ya Ihefu FC timu ambazo zinafukuzana kwenye msimamo, huku Dodoma FC ikikipiga na African Lyon na yoyote itakayofungwa inajikuta ikipoteza nafasi iliyokuwa sasa, na baada ya hapo Dodoma FC itacheza na Njombe Mji itakayokuwa nyumbani na katika mchezo uliopita Njombe iliilaza Ihefu na kuharibu msimamo wakati Ihefu ikikipiga na Boma FC.

Kwenye Kundi B, moto utawaka wakati Gwambina ikiikaribisha Geita huku wakiwa wamepishana alama tatu na endapo Gwambina wakifungwa wataweka rehani nafasi, baada ya hapo Gwambina itacheza na Sahare wakati Arusha FC ikicheza na Gipco FC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Geita Gold itaendelea kuwa na kazi ngumu kwani mchezo wake wa 17 watakuwa Arusha kucheza na AFC ambao katika michezo saba ya nyumbani wamepoteza mmoja kwa kufungwa 3-1 na Gwambina huku mingine ikishinda na zimepishana alama mbili.