Mchuano mkali... Van Dijk azua mjadala mzito England

LONDON, ENGLAND. MJADALA mzito. Nani beki bora wa muda wote kwenye Ligi Kuu England kati ya Virgil van Dijk na Nemanja Vidic. Wawili hao wanaonekana kutawala mjadala huo wa kuhusu beki wa kati bora kwa muda wote kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England. Sawa, kuna mabeki wengine kama John Terry, Rio Ferdinand na Tony Adams waliokuwa bora pia.

Lakini, mashabiki wameonekana kuvutiwa zaidi na mjadala wa kuhusu mabeki wa kigeni, Van Dijk na Vidic. Baada ya staa wa zamani wa Liverpool, Danny Murphy kudai katika kipindi cha televisheni cha Match of the Day 2 kwamba Mdachi Van Dijk ni beki bora wa kati aliyewahi kumshuhudia kwenye ligi hiyo, mjadala umeibuka upya.Murphy aliambia MOTD2: “Liverpool itakwenda kuwa dhaifu sana kwenye beki kwa kucheza bila ya Van Dijk kwa sababu ni beki bora duniani.

“Ni beki bora zaidi niliyewahi kumwona. Ni mzuri yaani.”

Jambo hilo limeibua mjadala kuhusu nani bora baina ya Van Dijk na Vidic. Kwa upande wa mataji, Vidic yupo juu ameshinda Ligi Kuu England mara tano katika miaka yake tisa aliyoichezea Manchester United. Akiwa na misimu miwili tu mizima kwenye kikosi cha Liverpool, Van Dijk amenyakua taji la ligi mara moja, lakini pia la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kingine kinachojadiliwa ni kwamba Mdachi huyo alitua Anfield wakati kukiwa na ukame wa muda mrefu wa mataji, huku Vidic alinaswa na Man United katika zama za Sir Alex Ferguson, alikutana pia na kipindi kigumu cha Chelsea ya Jose Mourinho iliyokuwa moto msimu wa 2005-06. Na wakati mabeki hao wawili wakishindanishwa kwa takwimu zao za Ligi Kuu England, ikumbukwe kuwa Van Dijk alitumikia miaka miwili na nusu ya mwanzoni England akiwa na kikosi cha Southampton. Van Dijk amecheza mechi 162 na Vidic mechi 211.

Kwenye mechi hizo, Van Dijk ameanzishwa mara 161 na Vidic mara 205, huku Mdachi akifunga mabao 14 na Mserbia akifunga 15. Van Dijk ana wastani wa kupiga pasi 68 kwa mechi huku Vidic akipiga pasi 47. Vidic amecheza mechi 95 bila ya kuruhusu bao, huku Van Dijk akicheza 61. Kwenye mechi hizo, Van Dijk ameruhusu mabao 153, wakati Vidic aliruhusu mabao 144. Mjadala huo umenoga zaidi baada ya mmoja wa mabeki ambao wangepaswa kuchuana, Vincent Kompany kuamua kumtaja mmoja, wakati alipoiambia Sporf: “Ningemchagua Virgil van Dijk tuzo ya beki bora wa kihistoria kwenye Ligi Kuu England. Ni chaguo la kushangaza kwa sababu hayupo kwenye anga moja na wakali kama Terry na Ferdinand.

“Wawili hao wamecheza kwenye ligi kwa muda mrefu sana, lakini dalili zote zimeonyesha kwamba Van Dijk yupo kwenye ligi kwa misimu michache sana na ameonyesha kubwa bora kuliko waliopita.”

Mjadala huo kwa upande wa mashabiki waliamua kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii walionekana kuungana mkono na wachezaji waliocheza kwenye timu zao.

Shabiki mmoja wa Chelsea aliandika kwenye Twitter: “Hebu tuache kuchanganya mambo Terry, Vidic na Rio wapo viwango vya juu kuliko Van Dijk.”

Wakati huohuo, shabiki wa Liverpool aliandika: “Van Dijk ni beki bora wa kati kirahisi sana. Hakuna beki wa kati kwenye Ligi Kuu England aliyeleta madhara makubwa kwenye timu kama VVD alivyofanya Liverpool. Kupoteza mechi tano katika misimu mitatu ni rekodi za kipekee sana. Anaweza asiwe na mataji mengi kama wapinzani wake Vidic, Terry au Rio lakini ni beki bora wa muda wote.”

Lakini, shabiki mmoja wa Man United alisema: “Van Dijk hawezi kabisa kuwakaribia Vidic na Terry, anaonekana bora kwa sasa kwa sababu hakuna mabeki wa maana, hakuna mabeki wa kati wa kiwango cha dunia.”