Mbwana Samatta alivyofanyiwa vipimo Fenerbahce

 Mshambuliaji wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta alitua jijini Istambul nchini Uturuki, wiki iliyopita katika klabu ya soka ya Fenerbahce inayokipiga Ligi Kuu.

Samatta mwenye umri wa miaka 27 ametokea katika klabu ya Aston Villa ya England iliyoamua kumtoa kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Kama ilivyokuwa kwa Aston Villa, Samatta alifanikiwa kufuzu vipimo vya afya vilivyofanyika jijini Istambuli katika kituo cha uchunguzi wa utimamu wa mwili kwa wanamichezo na kupeta.

Kilichosubiriwa baada ya hapo ni kuanza rasmi kukipiga katika ligi hiyo ambayo ni moja ya zenye timu kali ambazo zina upinzani wa hali ya juu. Siku zote moja ya kikwazo cha mchezaji kutua klabu nyingine ni pale afya mwili inapobainika haikuwa timamu.

Leo nitawapa ufahamu wa mchakato huu wa upimaji ambao unaweza kubaini matatizo ya kiafya, kimwili na kiakili yanayoweza kumnyima dili mchezaji kama Samatta.

UCHUNGUZI UKO HIVI

Kwa kawaida uchunguzi hufanyika katika vituo maalumu vya kisasa vyenye vifaa na huweza kuchukua takribani kati ya saa 12-24 iwapo taratibu kamili zitafuatwa.

Uchunguzi huo hutegemeana na umri na afya - kiujumla na historia ya familia na mienendo pamoja na mitindo ya maisha ikiwamo kama mwanamichezo anatumia tumbaku au kilevi chochote.

Samatta hatumii kilevi chochote wala kuvuta au kutumia bidhaa zitokanazo na tumbaku jambo ambalo lilikuwa na faida katika mchakato huu. Uchunguzi hujikita kuangalia zaidi matatizo ya mfumo wa moyo na mzunguko wa damu, mfumo wa upumuaji, fahamu, mifupa, misuli na mengineyo.

Uchunguzi unaweza ukaanzia katika historia ya mwanamichezo kama ana dalili zozote au historia ya magonjwa sugu au ya kurithi katika familia.

Vilevile uchunguzi wa kimwili ikiwamo upimaji wa shinikizo la damu, kasi ya upumuaji, joto la mwili na msukumo wa damu katika mshipa. Vipimo vya uzito, urefu na upimaji wa ukubwa wa misuli mikubwa ya mwili pia hufanywa kubaini uzito mkubwa au mdogo.

Vipimo vya kisasa hutumika kuweza kubaini matatizo ya kiafya yaliyojikita ndani zaidi ikiwamo vipimo vya picha za CT na MRI

Kwa upande wa uchunguzi wa mwili unaweza ukahusisha maabara na vipimo vya picha.

Vipimo kama vya wingi wa damu na kundi lake, kipimo cha picha nzima ya damu, kiwango cha sukari ya mwili, vipimo vya maambukizi ya magonjwa ya kujamiana na ukimwi.

Vilevile uchunguzi wa picha za mwili ikiwamo ya kifua ya xray, vipimo vya uchunguzi vya moyo ikiwamo kipimo cha picha ya moyo na cha kuona ufanyaji kazi wa moyo.

Shirikisho la Soka duniani (Fifa) liliamua kuweka mwongozo wa uchunguzi wa kiafya wa kina wa moyo hasa baada ya matukio ya wanasoka kuanguka na kufariki dunia viwanjani.

Uchunguzi wa moyo ni muhimu sana, kwani inahofiwa endapo mchezaji atakuwa anashiriki michezo matatizo katika mfumo wa damu na moyo huweza kusababisha moyo kusimama na kupata kifo cha ghafla.

Uwepo wa magonjwa ya moyo unamweka mwanamichezo katika hatari ya kuweza kudondoka na kuzimia uwanjani na pengine kupoteza maisha.

Majaribio mbalimbali ambayo hufanyika katika maabara maalumu ambazo huwa na mashine za kukimbilia huweza kubaini kasi ya mwanamichezo huyo kama anakidhi kasi inayotakiwa awe nayo - anayo.

Vilevile hufanyiwa majaribio ya mazoezi ya viungo kuona uimara wa mwili kiujumla, uwezo wake wa kuona, kutumia akili na kufanya uamuzi.

Wataalamu wa afya za wanamichezo ndio wanawagundua wanamichezo kama kasi na viwango vimepungua na hatimaye huchukuliwa kuwasaidia ili kurudisha viwango vyao.

Uchunguzi huweza kubaini uwapo wa majeraha ya mara kwa mara yasiyopona, hivyo kumpunguzia mwanamichezo ufanisi na kiwango. Ugunduzi wa hili unasaidia kumpa ushauri na matibabu ya majeraha.

Uchunguzi wa kiafya ndio huweza kubaini mchezaji kama ana uzito mkubwa au mdogo na uimara wa misuli unapungua katika eneo fulani mwilini.

Kwa wale wenye uzito mkubwa huweza kupewa ushauri wa namna ya kudhibitii uzito wa mwili ikiwamo kushauriwa kuacha kula vyakula vya mafuta mengi, wanga na sukari kwa wingi.

Uchunguzi huu huweza pia hubaini kasoro za kimaumbile ya mwili ambazo zinaweza kumfanya mwanamichezo kuwa wa kiwango cha kimataifa.

Wataalamu wa afya huwa na uwezo wa kugundua matatizo ya kisaikolojia na kitabia kwa wachezaji ikiwamo ulevi uliopindukia, uvutaji sigara na mifarakano ya kifamilia,

hivyo wanapogundua hili huweza kuchukua hatua ikiwamo kuwapa tiba ya kurekebisha tabia hizo.

Uchunguzi wa kiafya pia huweza kubaini mchoko hasa baada ya mwanamichezo kutumika kupita kiasi.

Kwa kawaida wanasoka wanapotoka kushiriki katika mashindano mbalimbali au wakati wa safari ndefu au mazoezi makali hupata hali ya uchovu.

Uchunguzi wa kiafya wanaofanyiwa ndio unaotoa mustakabali wa mwanasoka kununuliwa na klabu au kupewa mkataba kwa mkopo kama ilivyo sasa kwa Samatta. Hata hivyo Samagol amepeta katika kikwazo hiki cha uchunguzi wa utimamu wa afya na ni matarajio ya mashabiki wa timu hiyo kuwa ataibeba.