Mbeya Dabi haina kuremba

Friday August 23 2019

 

By Yohana Challe

LAZIMA kiwake. Ligi Kuu Bara inafunguliwa rasmi kesho Jumamosi, lakini mashabiki wana hamu ya kusikia kitakachojiri kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati Mbeya City na Tanzania Prisons zitakavyokiwasha huku kila timu ikipania kumaliza kazi mapema.

Msimu uliopita Tanzania Prisons ikiwa mwenyeji ililala mabao 2-1, kisha kwenye marudiano ilipindua meza na kushinda 1-0 bao la Salum Kimenya dakika ya 70.

Rekodi zinaonyesha tangu msimu wa 2015/16 Prisons imeitawala Mbeya City, kwani katika michezo minane ya Ligi Kuu, imeshinda minne akianza kwa 1-0 Septemba 15, 2015, kisha Januari 28, mwaka 2017 akishinda 2-0, Januari 14 mwaka jana akipata ushindi wa mabao 3-2, na mapema mwaka huu akivuna tena ushindi wa bao 1-0. Mbeya City imevuna ushindi mmoja pekee wa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa ligi msimu uliopita yaliyofungwa na Peter Mapunda dakika ya 7 na lile la Erick Kyaruzi dakika ya 87 wakati bao la kufutia machozi la Prisons likifungwa na Jeremia Juma dakika ya 41 huku michezo mitatu wakitoka uwanjani kwa suluhu.

Kocha wa Prisons, Mohammed Rishard Adolf alisema; “Utakuwa mchezo wa ushindani kwa sababu wote tunajuana na tupo hapa na ukiangalia kikosi chetu hatuna mabaya zaidi ya kufanya maandalizi mazuri.”

Adolf aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitahidi kuisapoti timu yao kwa maana wote wanawajibu wa kuhakikisha Prisons inapata matokeo mazuri na kufika mbali kwenye Ligi Kuu msimu huu bila kujali wapo ugenini au nyumbani.

Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi aliyekipandisha kikosi hicho msimu 2012/13 Ligi Kuu kabla ya kuondoka na kurejea msimu huu, alisema wanaendelea kujinoa kuelekea katika mchezo huo.

Advertisement

“Tumekamilisha maandalizi yetu na hakuna majeruhi ambao wangetuathiri, hivyo tunasubiri siku ifike na tuweze kupambana ili kupata matokeo mazuri,” alisema.

Advertisement