Mbeya City kuipima Dodoma Mji

Muktasari:

Miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa kutoka timu za ligi kuu ambao watacheza mbele ya mashabiki wa timu hiyo leo ni kipa Emmanuel Mseja aliyetokea Simba, Ali Ahmed Shiboli kutokea JKT Tanzania, Kassim Kilungo kutokea Tanzania Prisons, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyetokea Ruvu Shooting.

BAADA ya kukamilisha usajili wa wachezaji 26 watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao, timu ya Dodoma Jiji inacheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Mbeya City leo Jumamosi.
Mchezo huo ambao ndio kipimo cha kwanza kwa timu hiyo tangu ilipoanza mazoezi utachezwa katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa ukiwa wa kujipima uwezo wakati huu ikijiandaa na hekaheka za ligi daraja la kwanza.
Miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa kutoka timu za ligi kuu ambao watacheza mbele ya mashabiki wa timu hiyo leo ni kipa Emmanuel Mseja aliyetokea Simba, Ali Ahmed Shiboli kutokea JKT Tanzania, Kassim Kilungo kutokea Tanzania Prisons, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyetokea Ruvu Shooting.
Wengine ni Joseph Simbaulanga kutokea Biashara United, Jamal Mtegeta na Rajabu Kibela waliotokea Alliance, Hassan Kapona na Abubakar Ngalema waliotokea timu ya Mbao zote za Mwanza.
Chini ya Kocha wake Mbwana Makatta, Dodoma Jiji imepangwa kundi A la ligi hiyo ikiwa na timu za Friends Rangers, Ashanti United, African Lyon, Ihefu, Boma, Majimaji, Mbeya Kwanza, Mlale JKT, Mufindi United, Reha na Njombe Mji.
Katibu wa timu hiyo, Fortunatus John alisema mchezo dhidi ya Mbeya City ni kipimo kizuri kwao na wanatarajia kucheza mechi nyingi za kirafiki za ndani na nje ya Dodoma yenye lengo la kukiweka sawa kikosi hicho.
“Tutacheza mchezo maalum wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wetu Jamhuri kabla ya kuangazia mechi nyingine zijazo za kirafiki ambazo tutazicheza kwa lengo la kukipima kikosi chetu kabla ya kuanza kwa ligi,” alisema John.
Ligi daraja la kwanza inatarajiwa kuanza Septemba 14 ambapo hata hivyo ratiba ya mechi za ufunguzi wake bado haijatoka ambapo Dodoma Jiji itampambana kwa mara nyingine kuisaka ligi kuu baada ya kushindwa misimu miwili iliyopita.