Mbelgiji shangwe kama lote Msimbazi

Muktasari:

  • Kocha wa Simba Patrick Aussems amesema kwamba kukosekana kwa wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza katika mechi na Stand United haikuwa shida kwani aliwamini ambao watakwenda kucheza katika nafasi hizo watafanya kazi ipasavyo.

SIMBA wamerejea ndani ya Tatu Bora ya Ligi Kuu Bara, lakini Kocha Mkuu wake, Patrick Aussems ni kama hajaridhika, huku akisisitiza kikosi chake hata akikosekana nani, bado wanaweza kumpiga yeyote ndani na nje ya nchi.

Aussems aliyasema hayo baada ya mechi yao dhidi ya Stand United akiwa amewakosa nyota wanne wa kikosi cha kwanza Jonas Mkude aliye majeruhi, Erasto Nyoni, James Kotei na John Bocco wanaotumikia adhabu ya kifungo toka Shirikisho la Soka Tanzania.

“Simba imekamilika, hata akikosekana mchezaji bado waliopo wanafanya kazi na hii tumeifanya ili tumudu vishindo vya mechi yoyote inayokuja mbele yetu iwe ndani ama zile za kimataifa,” alisema Aussems.

“Juuko Murshid alicheza kuziba nafasi ya Nyoni, amefanya kazi kama nilivyotaka Said Ndemla alicheza nafasi ya Mkude na alionesha utulivu, vivyo hivyo kwa nafasi nyingine kuonyesha Simba imejianda kwa namna gani msimu huu.’

Katika hatua nyingine nahodha wa Simba, John Bocco aliyekosa mechi tatu kama adhabu yake inavyoeleza anatarajiwa kushuka uwanjani kesho dhidi ya Alliance.

Aussems alisema kurejea kwa Bocco katika timu yake itaongeza nguvu hasa safu ya ushambuliaji ambapo kipindi hiki wakiwa wanahitaji ushindi kwa kila mechi ili kutengeneza mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi na kutetea taji lao.