Mbelgiji awatwisha zigo Kwasi, Coulibaly

Muktasari:

Wachezaji Ally Salim, Mohammed Ibrahim, Muivory Coast Zana Coulibaly, Abdul Selemani, Yusuph Mlipili, Mghana Asante Kwasi na Paul Bukaba wote wameachwa visiwani Zanzibar kuendelea na mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Dar es Salaam. Mabeki wa Simba, Zana Coulibaly, Asante Kwasi na wengine watano walioachwa Kisiwani Zanzibar, wamepewa mtihani mzito na Kocha Mbelgiji Patrick Aussems kuhakikisha wanafika fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
Aussems amefichua jioni hii kuwa amefanya uamuzi mgumu wa kuwaacha nyota hao hasa wanaocheza nafasi za ulinzi badala ya kuja nao Dar es Salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya JS Saoura kwa sababu anataka kuona Simba inatwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.
Amesema anaamini wachezaji hao waliobaki Zanzibar watafanya kazi hiyo aliyowatuma na baada ya hapo mabeki wawili watarudi Dar es Salaam ili kuziba nafasi iwapo kutatokea majeruhi wa dakika za mwisho.
"Mkakati wetu ni kufanya vizuri kwenye mechi yetu inayofuata dhidi ya JS Saoura lakini pia tuna mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambalo tumepanga kulichukua,"alisema Aussems na kuongeza.
"Hivyo nimeamua kuwaacha baadhi ya wachezaji kule kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali na baada ya hapo kuna wachezaji wengine wawili wa nafasi ya ulinzi watarejea Dar es Salaam kuungana na timu."