Mbelgiji amuumbua Zahera

Friday February 14 2020

 

By Charity James

HABARI ndio hiyo. Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ni kama amekuja kumuumbua aliyekuwa kocha wa zamani wa timu hiyo, Mwinyi Zahera kutokana na mfumo anaoutumia sasa na aina ya matokeo anayoyapata tangu aanze kukinoa kikosi hicho.

Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 38 imeonekana kubadilika kiuchezaji baada ya raia huyo wa Ubelgiji kumpokea Charles Boniface Mkwasa aliyekuwa akishikilia kwa muda kiti hicho kilichooachwa wazi na Zahera aliyetimuliwa Novemba mwaka jana.

Vijana wa Eymael kwa sasa wanaonekana kama walioupotezea kabisa mfumo aliokuwa anatumia Zahera wa 4-2-3-1 ambapo mshambuliaji mmoja alikuwa akisimama pekee yake, huku Eymael akitamba zaidi na ule wa 4-4-2 ambapo mashambulizi hutokea zaidi kwa mawinga wa pembeni. Pia, Yanga kwa sasa inaonekana kucheza soka la kuvutia lenye malengo tofauti na ilivyokuwa chini ya Zahera aliyewafanya mashabiki kuwa na presha, hasa walipokosekana Hertier Makambo na Ibrahim Ajibu.

Mfumo huo wa Eymael umesababisha baadhi ya nyota hao kuanzia benchi au kukosa namba kabisa tofauti na alipokuwepo Zahera ambaye alikuwa akiwatumia.

Waliopoteza namba kutokana na mabadiliko ya mfumo ni Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye alikuwa akitumiwa kama beki namba mbili na kumuweka benchi, mkongwe Juma Abdul ambaye alikosa namba kikosi cha kwanza kutokana na kiwango alichokuwa akikionyesha chipukizi huyo.

Chini ya Eymael, Boxer hana namba kikosi cha kwanza pamoja na kutoka majeruhi lakini tangu amejiunga na timu hiyo na kuanza mazoezi bado hajamshawishi kumpa nafasi ya kucheza.

Advertisement

Mrisho Ngassa alikuwa ni mchezaji namba moja kwa Zahera akitumika kama winga wa pembeni mwenye kasi ambaye alikuwa anamlisha mipira David Molinga lakini kwa sasa hajapata nafasi ya kucheza, sawa na ilivyo kwa winga mkali wa kigeni, Patrick Sibomana.

Upande wa beki mkongwe, Kelvin Yondani hakuwahi kukaa nje chini ya Zahera akikosekana basi ana kadi lakini muda wote alikuwa akipewa nafasi na kuaminiwa kutokana na uzoefu wake lakini sasa Eymeal amekuja na msimamo wake kwamba atakayefanya vizuri mazoezini ndiye atakayepata nafasi ya kucheza.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha licha ya Zahera kuiongoza Yanga kwenye mechi nne tu msimu wa ligi akivuna pointi 7 kwa kushinda mechi mbili na kutoka sare moja na kupoteza moja huku akikusanya mabao sita ya kufunga na kuruhusu matatu. Eymael ameiongoza Yanga katika mechi saba na kushinda nne na kutoka sare moja na kupoteza mbili, akifunga mabao manane na kufungwa sita, lakini mkali wao ni Mkwasa aliyeiongoza Yanga katika michezo nane na kukusanya alama 18 akiwa hajapoteza mchezo wowote zaidi ya sare tatu na kushinda tano, huku timu yake ikifunga mabao 11 na kuruhusu sita.

MAKAPU AFUFUKA UPYA

Said Juma ‘Makapu’ hakuwahi kuwa na namba chini ya Zahera sasa ameibuka na amekuwa akifanya vizuri zaidi nafasi ya beki wa kati ambayo ameonekana kuimudu vyema ambapo awali alikuwa akichezeshwa kama kiungo mkabaji.

Eymael ameamua kumtumia Makapu nafasi hiyo baada ya Yondani kutokuwepo kikosini kwa madai ya kuumwa na hajacheza mechi hata moja tangu kutua kwa kocha huyo.

Jaffar Mohammed ambaye enzi za Zahera alikosa namba kikosini humo, tangu enzi za Mkwasa alipewa shavu na kumpoteza kabisa Ally Mtoni ‘Sonso’ aliyekuwa akitumika enzi za Mkongoman kama beki wa kushoto.

Winga Deus Kaseke naye hakuwa na nafasi kwa Zahera, lakini baadaye akaibuliwa upya na Mkwasa amekuwa ni mmoja kati ya wanaoaminiwa na Eymael kwani mechi tatu alizocheza siku za nyuma alitoa pasi za mabao na kufunga bao moja.

WAFUNGUKA

Makapu alisema ni mapema sana kuzungumzia nafasi aliyopewa ila anashukuru kuaminiwa kwenye kikosi cha kwanza na kufiti mfumo wa mwalimu kutokana na kuchezeshwa nafasi mpya kwake.

Kaseke na Jaffar walisema kujituma na kutokata tamaa wakiamini ipo siku atapewa heshima kikosini hapo ndio siri yao.

Advertisement