Mbappe kawatia wazimu Liverpool

Muktasari:

  • Matukio kama hayo ndiyo yanayowafanya Liverpool kuamini kwamba huenda mbele ya safari huko kama si dirisha hili basi lile lijalo watafanikiwa kuinasa huduma ya moja ya wachezaji bora kabisa kwenye dunia ya soka kwa sasa.

LIVERPOOL, ENGLAND. SUPASTAA, Kylian Mbappe amewafanya mashabiki wa Liverpool kuishi na matumaini kwamba pengine fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa anavutiwa na mpango wa kujiunga na timu yao huko Anfield.

Mbappe amekuwa akihusika kwenye matukio mbalimbali yanayoihusisha Liverpool ambayo huenda yakamzindua kocha Jurgen Klopp na kuamua kupeleka ofa ya kutaka huduma ya mshambuliaji huyo matata kabisa kwenye dunia ya mchezo wa soka kwa sasa.

Sawa, Mbappe hatarajiwi kuondoka Paris Saint-Germain katika dirisha hili la majira ya kiangazi huku Liverpool nao wakionekana kutokuwa na dhamira ya kutumia pesa nyingi baada ya kuwanasa Alisson na Virgil van Dijk katika madirisha yaliyopita.

Lakini, mambo ya Mbappe ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia yamewafanya Liverpool kuwa na imani baada ya hivi karibuni kuonekana akiwa na staa wa mpira wa kikapu, LeBron James, ambaye ni shabiki mkubwa wa Liverpool huku kwenye video yao waliwa pamoja, kofia yenye nembo ya Liverpool ilikuwa ikionyeshwa.

Mashabiki wa Liverpool wamepata mzuka zaidi baada ya kumwona staa huyo wa PSG akianza kuwafolo mastaa wa zamani na wasasa wa kikosi hicho cha Anfield kwenye mtandao wa Instagram.

Matukio kama hayo ndiyo yanayowafanya Liverpool kuamini kwamba huenda mbele ya safari huko kama si dirisha hili basi lile lijalo watafanikiwa kuinasa huduma ya moja ya wachezaji bora kabisa kwenye dunia ya soka kwa sasa.

Mbappe aliwahi kuhojiwa hivi karibuni na mtangazaji wa ESPN, Mauricio Pedroza alipoulizwa ni timu gani atapenda kuicheza kwenye gemu ya FIFAM staa huyo alijibu "Liverpool."

Alidai kwamba ameichagua timu hiyo kwa sababu imetoka kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akimtaka kocha Klopp kuwa ni bora. Hata hivyo, vyovyote itakavyokuwa, Liverpool hawaonekani kama wataweza kumnasa Mbappe kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi alisema: "Mbappe? Nina hakika kwa asilimia 200 atabaki kwenye kikosi cha PSG msimu ujao."