Mbao yacheza dakika 360 bila ushindi Ligi Kuu

Tuesday December 4 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Matokeo ya juzi dhidi ya Ndanda, yameifanya Mbao FC kufikisha dakika 360 bila kupata ushindi katika mechi nne mfululizo.

Mbao juzi ilitoka suluhu na Ndanda katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Mara ya mwisho timu hiyo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Akizungumza jana, Kocha Msaidizi wa Mbao, Almas Moshi alidai matokeo hayo siyo mazuri kwa kuwa yanaiweka timu hiyo katika mazingira magumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Moshi alisema baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi nne, wamejipanga kucheza kufa au kupona ili kupata matokeo mazuri katika mchezo ujao dhidi ya Africa Lyon.

African Lyon itacheza mchezo huo ikiwa na maumivu, baada ya kucharazwa mabaao 4-1 na Mbeya City katika mchezo wa juzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

“Kila mchezo tunajipanga vizuri kushinda, lakini ndiyo hivyo mpira una matokeo matatu, lazima tukubaliane nayo kikubwa kwa sasa tunaelekeza nguvu katika mechi yetu na Lyon kuhakikisha tunashinda,”alisema Moshi.

Kocha huyo alidokeza mchezo wa Desemba 10 utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, utakuwa ni vita kwa kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo watatumika kupata pointi tatu.

“Kuna wachezaji wanne ambao tumeongeza huenda mechi ijayo wakapata nafasi kwahiyo mashabiki wetu watuunge mkono bila kukata tamaa, lengo letu ni kuhakikisha tunakaa nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu,”alisema Moshi.

Mbali na mchezo wa juzi, Mbao ilichapwa mabao 3-1 na Lipuli, ilitoka sare 2-2 na Mbeya City kabla ya kutoka suluhu na Biashara United.

Advertisement