Mbabe wa Simba hatihati kuikosa

Wednesday September 16 2020

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Biashara United inayojiandaa kuivaa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu, Simba, straika wa timu hiyo, Gerald Mathias amesema bado hajajihakikishia kucheza mechi hiyo kutokana na majeraha aliyopata kwenye mchezo uliopita.

Biashara United imekuwa na mwanzo mzuri msimu huu kufuatia ushindi wa mechi mbili mfululizo ilizocheza katika uwanja wa nyumbani, ambapo kwa sasa wanajiandaa kuwafuata Simba - pambano litakalopigwa Jumapili, wiki hii.

Iwapo nyota huyo atawakosa Wekundu hao itakuwa faraja kwao kwani msimu uliopita ndiye aliwaliza mapema wakati akiisaidia timu yake ya zamani, Mwadui FC kushinda kwa bao 1-0 mjini Shinyanga.

Mathias aliumia wakati timu yake ikipambana dhidi ya Mwadui FC, ambapo licha ya kuisaidia timu kushinda bao 1-0, lakini alijikuta akimaliza mchezo na maumivu baada ya kuumia nyama za paja.

Akizungumza na Mwananchi, mshambuliaji huyo alisema hadi sasa ni vigumu kuthibitisha kama ataivaa Simba, kwani bado hayupo sawa na huenda akaikosa mechi hiyo.

Alisema kukosa mechi kubwa kama hiyo ni pigo kwani ni aina ya michezo inayompandisha mchezaji, hivyo itakuwa maumivu makubwa iwapo ataukosa mpambano.

Advertisement

“Mechi kama hizo huwa na faida kubwa sana, zinaweza kukupandisha mchezaji, hivyo kuikosa ni hasara kubwa lakini sina namna lazima nikubaliane na matokeo.”

Advertisement