Maswali 10 tata ishu ya Morrison

KWA mujibu wa kauli za wadau mbalimbali kuna ugumu kwenye sakata jipya waliloliibua Yanga dhidi ya Mghana, Bernard Morrison.

Yanga juzi waliibuka na mkataba wa kazi ambao wanadai ndio uliomhalalisha Morrison Simba huku ukiwa hauna saini yoyote ya uongozi zaidi mchezaji huyo na wanadai ndio uliotumwa na Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) kwenye mtandao kuhalalisha achezee Msimbazi.

Rais wa TFF,Wallace Karia alisisitiza jana kufuatilia kwa kina sakata hilo, lakini Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Kasanda Mitungo amedai kuwa kama mkataba ulioonyeshwa na Yanga juzi ndiyo uliompa uhalali mchezaji huyo kucheza Simba, basi leseni yake ni batili.

Juzi makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alidai wameupata mkataba wa Simba na Morrison aliyewahi kuitumikia Yanga kwa miezi sita kabla ya kujiunga na Simba msimu huu wa dirisha kubwa.

Yanga na Morrison waliingia kwenye mgogoro wa kimkataba, baada ya klabu hiyo kumjumisha kwenye orodha ya wachezaji wake wakati wa dirisha kubwa ikisisitiza imemuongezea mkataba wa miaka miwili ambao mchezaji aliukana.

Kamati ya sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF ilisema Morrison ni mchezaji huru ikidai mkataba wake na Yanga ulikuwa na mapungufu na mchezaji huyo kujiunga na Simba siku chache baadae na Yanga ikitishia kupeleka suala lao CAS.

Karia amesema; “Msimamo wa TFF ni ule ule, suala la Morrison kama tulivyosema tunalifuatilia na tukikamilisha tutalitolea tamko."

Akizungumza kisheria jana, wakili Kasanda alisema pamoja na kwamba mkataba huo unaihusu Simba na Morrison, Yanga ina haki ya kuulalamikia kwa kuwa ni mdau.

"Kama ni kweli,mkataba unaoonyeshwa na Yanga kuwa ndiyo uliompa uhalali Morrison kucheza Simba, kama ndiyo mkataba halisi, basi una mapungufu na leseni iliyotolewa kwa kutumia mkataba huo nayo ni batili,"alisema.

Licha ya kwamba mwanasheria na Naibu waziri wa mambo ya nje, Damas Ndumbaro amesisitiza kuwa wanaoweza kulalamika kwenye mkataba huo ni wale ambao ni sehemu ya mkataba na Yanga hawawezi kulalamika popote sababu si sehemu ya mkataba ule, Kasanda amekuwa tofauti akibainisha kwamba, Yanga ananafasi ya kulalamika kama mdau katika Ligi.

"Mkataba kama ni ule ambao Yanga wanadai ndiyo Morrison ameingia na Simba, basi utakwenda kuathiri hadi Ligi,kwani klabu itakuwa imemtumia mchezaji ambaye usajili wake haujakamilika kwa kuwa mkataba ule unaonekana ni wa upande mmoja," alisema mwanasheria huyo wa kujitegemea.

Alisema cha msingi ni kujua uhalali wa mkataba ule ambao Yanga wameuonyesha kuwa ni wa Simba na Morrison kama ndiyo huo huo ambao huko TFF, kama ndivyo basi leseni iliyotolewa kwa kutumia mkataba ule ni batili.

Ingawa Mwenyekiti wa kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji wa TFF, Elias Mwanjala alipoulizwa juu ya uhalali wa mkataba huo alisema halijafika mezani kwao kama kamati lakini wakiletewa watalishughulikia kwavile ndiyo majukumu yao.

"Mkataba ni makubaliano lakini sio makubaliano yoyote ni mkataba,katika sheria ya mkataba kifungu cha 10, kinaeleza uhuru wa mtu kuingia katika makubaliano, ukiachana na umri, akili, kibali cha kufanya kazi, lakini sahihi inaleta nguvu na ni sehemu muhimu kuwepo kwenye mkataba kati ya pande mbili," alisema Kasanda.

"Kama mkataba haujakamilika,leseni ilitokaje? hivyo klabu nyingine zina haki ya kuhoji sababu zinaathirika kwa kumtumia mchezaji ambaye usajili wake haujakamilika, ikithibitika lazima hatua zichukuliwe.

Ingawa Ndumbaro amesema wa kulalamika katika mkataba ule ni Simba au Morrison.

Makamau mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema ukiachana na sakata lao na Morrison, walimkatia rufaa mchezaji huyo na haikusikilizwa.

"Tuliambiwa kulikuwa na mapungufu ya kimkataba kati ya klabu na mchezaji, lakini mapungufu hayo hayo yameonekana kwenye mkataba baina ya mchezaji huyo huyo na Simba.

"Japo mkataba ni siri ya muajiri na mwajiriwa lakini tumeupata ni mkataba na tuliwatumia TFF huo mkataba wa Simba na kuwataka waupitie upya, lakini hawakutujibu ndiyo sababu tumeamua kusema hadharani kinachoendelea,".

Uongozi wa Simba ulipotafutwa jana ili kuzungumzia mkataba huo hakuna aliyepokea simu siku nzima ya jana.

MASWALI 10 TATA

1. Je,mkataba huo  ulioanikwa na Yanga ni sahihi na sawa na ule uliopo TFF baina ya Simba na mchezaji au sio wenyewe?

2. Kama ni sahihi, Je, kweli mkataba huo baina ya Simba na Morrison uliowasilishwa TFF hauna saini za upande wa Simba kama ilivyodaiwa au hakuna ukweli katika hilo?

3. Lakini ikithibitika kama mkataba huo ni sahihi na ni kweli hauna saini za upande wa Simba, kwa nini TFF iliupokea na kuupitisha kisha kumpa leseni mchezaji huyo kuichezea Simba msimu huu?

Kanuni za Ligi Kuu msimu huu, zimefafanua wazi kuwa mchezaji hatocheza Ligi bila kuwa na leseni inayotolewa na TFF na leseni haiwezi kutolewa ikiwa mkataba baina ya mchezaji husika na klabu haujapitia mikononi mwa shirikisho na kupitishwa.

"Wachezaji wote watatambulika kwa kutumia Leseni zao zitakazotolewa na kuidhinishwa na TFF.   Mchezaji yeyote ambaye   hatakuwa na leseni hatoruhusiwa kucheza katika mchezo husika," inafafanua ibara ya 17 ya kanuni ya 15 ambayo ni taratibu za mchezo.

Lakini kanuni ya 63 imefafanua utaratibu wa usajili na pia utoaji wa leseni kwa wachezaji.

"Klabu zinawajibika kutumia mikataba elekezi iliyotayarishwa na TFF kuhamisha, na kusajili wachezaji wake, mikataba mingine yote haitatambulika. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ndio chombo kilicho na mamlaka ya  kushughulikia  masuala  ya  usajili,  kuthibitisha  au  kutengua  usajili  wa  mchezaji," inafafanua ibara ya tatu (3) na ile ya 14 ya kanuni ya 63.

4.Pamoja na hilo, pia hoja nyingine inayoibuliwa hapo ikiwa ni kweli mkataba haukusainiwa upande wa Simba ni kwa nini uongozi wa timu hiyo uliamua kufanya hivyo wakati ni kitendo kinachoufanya mkataba uwe batili ukizingatia kosa kama hilo ndilo lilipelekea Morrison awe mchezaji huru licha ya Yanga kudai kuwa ina mkataba naye? Na kwanini viongozi rasmi wa Simba wakiongozwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez wapo kimya mpaka sasa?

Kanuni ya 45 ya udhibiti kwa klabu, imefafanua adhabu ambazo timu inaweza kupata ikiwa itabainika kuwasilisha mkataba wenye kasoro itachukuliwa hatua za kinidhamu.

"Timu iliyomchezesha mchezaji aliyethibitishwa usajili wake lakini   aliyebainika  kubadili  jina  kwa  nia  ya  kudanganya  au kubainika kutumika udanganyifu  mwingine  wowote kufanikisha kukamilisha  usajili  wake  au  mchezaji aliyebainika usajili wake kuwa na kasoro baada ya kuthibitishwa italipa  faini  kati ya sh ilingi  laki  tano (500,000/-)  na sh ilingi  milioni  tatu (3,000,000/-)  kwa  kila  mchezo  aliocheza lakini matokeo  ya  uwanjani  hayatobadilishwa," inafafanua ibara ya 22 ya kanuni hiyo.

5. Je, ni nani aliyeipa Yanga mkataba huo hadi ikathibitisha kuwa ulikuwa na mapungufu wakati ni pande tatu tu ambazo kisheria zinapaswa kuwa nazo ambazo ni Simba kama muajiri, Morrison (Muajiriwa) na TFF kama msimamizi na chombo chenye mamlaka ya mwisho ya kusimamia masuala ya usajili wa wachezaji na mpira wa miguu hapa nchini.

6.Ukiondoa hilo, lingine ni, Je, kwa nini Yanga imeibuka na madai kwa sasa na haikufanya hivyo katika muda uliotengwa wa kuwasilisha mapingamizi ya usajili kama inavyofafanua kanuni ya 68.

"Klabu  yoyote,  FA(W),  FA(M)  na  mamlaka  nyingine  wanaweza  kuweka  pingamizi kupinga usajili wa mchezaji yeyote kwenye kipindi cha Pingamizi kitachowekwa na kutangazwa na TFF. Pingamizi ni lazima liwekwe katika kipindi maalum cha Pingamizi na lazima liwe  kwa  maandishi  kwa  TFF,  mwekaji  akiainisha  sababu  pamoja  na  kuambatanisha vielelezo husika," inafafanua kanuni hiyo.

Hata hivyo kanuni ya 70 imefafanua kuwa pingamizi lililowasilishwa nje ya muda husika litatupwa.

"TFF  haitotoa  manufaa  kwa  mlalamikaji  kwa  malalamiko  yoyote  kuhusu  usajili  kwa mchezaji  ambaye  usajili  wake  umethibitishwa  na  TFF  akiwa  hakuwekewa   pingamizi   la   usajili au   ambaye   Pingamizi   dhidi   yake   lilitatuliwa na Kamati," inafafanua ibara ya tatu ya kanuni hiyo.

7. Hoja nyingine inayoibuka ni uadilifu na umakini wa kamati za TFF kutokana na udhaifu kujirudia je, wanafanya kwa bahati mbaya makosa hayo ya usajili au makusudi?

Ikumbukwe ni huyohuyo Morrison, jina lake lilipitishwa achezee Yanga huku mkataba wake na klabu hiyo ukidaiwa kuwa na mapungufu.

8. Je, TFF itachukua hatua gani katika muendelezo wa udhaifu na makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na kamati yake inayohusika na masuala ya usajili ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na kusababisha migogoro isiyokwisha?

9. Yanga awali walidai hawana imani na kamati ya Sheria na hadhi za Wachezaji chini ya Mwanjala na kudai kwamba malalamiko yao kuanzia sasa watakuwa wakiyapeleka CAS na Fifa, iweje leo warudishe tena malalamiko kwenye kamati hiyohiyo?

10. Je,ni nini kitakwenda kutokea ikiwa itabainika madai ya Yanga ni ya msingi na pia iwapo hayatokuwa na msingi? Ikiwa ya msingi, nani wataadhibiwa kati ya Simba au maofisa wa TFF waliofanya makosa hayo lakini ikiwa hayatakuwa ya ukweli, uongozi wa Yanga utaadhibiwa kwa udanganyifu?

IMEANDIKWA NA IMANI MAKONGORO, MWANAHIBA RICHARD, CHARLES ABEL NA CHARITY JAMES