Mastaa wanaosubiriwa kwa hamu dirisha hili la usajili

LONDON, ENGLAND. GARETH Bale ameshakamilisha dili lake la uhamisho wa mkopo wa msimu mzima wa kujiunga na klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur. Kwingineko kwenye taarifa za usajili, kiungo Mhispaniola Thiago Alcantara amejiunga na Liverpool akitokea Bayern Munich huku wakala wa kipa Edouard Mendy akifichua mpango wa mteja wake kwenda kujiunga na Chelsea umeshakamilika kila kitu na kilichobaki ni muda tu wa kutangazwa kwa dili hilo.

Wakati mashabiki wakisubiri Oktoba 5 ifike ambayo ni mwisho wa usajili kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, kuna dili 10 ambazo wanasubiri kwa hamu kuona kama zitaweza kutiki.

JADON SANCHO

Kutoka: Borussia Dortmund

Kwenda: Man United

Ada: Pauni 108 milioni

United ilishindwa kukamilisha dili la kumnasa Sancho baada ya Borussia Dortmund kuwapa siku ya mwisho kuwa Agosti 10. Lakini, Man United imerudi tena kwenye mchakato wa kunasa saini hiyo ya winga Mwingereza huku ikiamini Dortmund itashuka bei wanayomuuza mchezaji huyo, Pauni 108 milioni.

KALIDOU KOULIBALY

Kutoka: Napoli

Kwenda: Man City

Ada: Pauni 70 milioni

Kwa muda mrefu, beki wa kati Kalidou Koulibaly amekuwa akiwindwa na klabu vigogo wa Ligi Kuu England kama Manchester United, Man City na Liverpool. Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Koulibaly amekuwa akihusishwa tena na mpango wa kuachana na timu yake huku Man City ikipewa nafasi kubwa ya kunasa huduma yake ili akakipige huko Etihad. Kocha Pep Guardiola amepewa siku za kuhakikisha anakamilisha dili la mchezaji huyo ambaye Napoli imedai hawatamuuza kwa ada isiyopungua Pauni 70 milioni.

HOUSSEM AOUAR

Kutoka: Lyon

Kwenda: Arsenal

Ada: Pauni 50 milioni

Nahodha wa Lyon, Aouar ameibukia kwenye mipango ya kocha wa Arsenal, Mikel Arteta akitaka huduma yake katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Arsenal inapiga hesabu pia za kwenda kumnasa kiungo wa Atletico Madrid, Thoomas Partey. Lakini, Arteta atapaswa kuuza wachezaji wasiopungua watatu kupata huduma ya Aouar, ambaye kocha alisema kama hatakuwa na bajeti ya kutosha basi chaguo lake la kwanza litakwenda kwa Aouar.

DECLAN RICE

Kutoka: West Ham

Kwenda: Chelsea

Ada: Pauni 45 milioni

Amekuwa moto wa kuotea mbali huko West Ham United. Bilionea mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich ametaa ruhusa ya kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha hili, ambapo tayari imeshanasa mastaa kama Kai Havertz, Ben Chilwell, Timo Werner, Hakim Ziyech na wengineo. Kocha Frank Lampard bado anataka kumwongeza Rice kwenye kikosi chake kwa ada ya Pauni 45 milioni.

LUIS SUAREZ

Kutoka: Barcelona

Kwenda: Juventus au Atletico

Ada: Pauni 13.5 milioni

Straika, Luis Suarez ameambiwa bayana na kocha Ronald Koeman hatamhitaji tena kwenye mipango yake huko Barcelona. Baada ya jambo hilo kutokea, Suarez alihusishwa na kwenda Ajax kabla ya Juventus kwenda kujaribu mpango wa kunasa huduma yake. Hata hivyo, mabingwa hao wa Italia wamemtolea macho Edin Dzeko, hivyo kumfanya Suarez sasa kuwindwa na Atletico Madrid.

MEMPHIS DEPAY

Kutoka: Lyon

Kwenda: Barcelona

Ada: Pauni 28 milioni

Winga wa zamani wa Manchester United, Memphis Depay amekuwa kwenye kiwango moto kabisa baada ya kutua katika kikosi cha Olympique Lyon ya huko Ufaransa. Kocha mpya wa huko Nou Camp, Ronald Koeman anamtaka Mdachi huyo, ambaye atamgharimu Pauni 28 milioni.

DELE ALLI

Kutoka: Tottenham

Kwenda: PSG au Inter Milan

Ada: Pauni 60 milioni

Kiungo Dele Alli amekuwa akifukuziwa na Paris Saint-Germain na Inter Milan baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba ametibuana na kocha Jose Mourinho huko Tottenham Hotspur. Kocha huyo alimtoa Dele Alli kwenye kipindi cha kwanza tu wakati Spurs ilipokutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Everton kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England na hakuhitaji huduma yake kwenye mchezo wa Europa League dhidi ya Lokomotiv Plovdiv.

SAMI KHEDIRA

Kutoka: Juventus

Kwenda: Man United

Ada: Bure

Kiungo huyo Mjerumani, Khedira akiwa na umri wa miaka 33 mkataba wake ulisitishwa huko Juventus mwaka mmoja kabla ya kufika mwisho baada ya miamba hiyo ya Italia kufanya usajili wa viungo wengine, Arthur na Weston McKennie. Na kinachoelezwa ni kwamba Man United imeonyesha dhamira ya kunasa huduma yake ya bure ambapo kocha Ole Gunnar Solskjaer akitaka kumwongezea mkongwe huyo kwenye kikosi chake ili kuwafanya makinda wake wengi kupata uzoefu wa kuhimili mechi mbalimbali zenye changamoto ya kupata ushindi.

DAVID BROOKS

Kutoka: Bournemouth

Kwenda: Man United au Leicester City

Ada: Pauni 50 milioni

Bournemouth imevamiwa na wachezaji wake kuchukuliwa tangu iliposhuka daraja, ambapo Callum Wilson na Ryan Fraser wameshaondoka na kwenda kujiunga na Newcastle United kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Baada ya hilo, staa wao David Brooks naye anaelekea kwenye mlango wa kutokea, ambapo Manchester United na Leicester City zinatajwa kusaka saini yake. Hata hivyo, Bournemouth imetaja bei ya mchezaji huyo hawezi kung’oka kwenye kikosi chao kwa ada isiyokuwa ya Pauni 50 milioni.

ISMAILA SARR

Kutoka: Watford

Kwenda: Liverpool au Man United

Ada: Pauni 36 milioni

Kama ilivyo kwa Bournemouth, Watford nayo ni klabu iliyovamiwa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi timu zikija kuchukua wachezaji baada ya kushuka daraja na sasa United na Liverpool zimeripotiwa kumtaka Ismaila Sarr. Liver inataka Sarr aende akawe chaguo la ziada la kutanua kikosi chao kuwasaidia Mohamed Salah na Sadio Mane, lakini United nao wana uhaba wa wachezaji wa pembeni.