Mastaa wa Man United wako spidi hao balaa!

Friday January 11 2019

 

 MANCHESTER United wamefanya kambi huko Dubai wakijifua kwenye hali ya hewa ya joto kujiweka fiti kabla ya kurudi England kumalizia msimu. Wakiwa kambini, kuna wachezaji wawili wa kikosi cha kwanza hawakuwapo, Marcos Rojo na kiungo wa Kibrazili, Fred.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alitoa sababu ya wakali hao kutokuwapo kambini, Rojo ikiwa ni majeruhi na Fred ni kwamba amerudi kwenye kusikilizia mkewe anatarajia kujifungua. Haya, shikilia hapohapo kwenye nukta ya kujifungua.

Unajua nini, kuna mchambuzi mmoja wa mambo ya soka alishawahi kuwaambia Manchester United: “Kamwe hamwezi kushinda chochote mkiwa na watoto.” Sawa, hilo lilikuwa na maana ya kuwa na wachezaji makinda.

Lakini, Man United wanaamini hilo haliwezi kujitokeza msimu huu, kwa sababu kwenye kikosi hicho kuna kundi la watoto litazaliwa mwaka huu.

Kiungo Fred ni mwanzo tu wa mastaa kibao, wasiopungua watano ambao wanatarajia kupata watoto ndani ya mwaka huu. Msimu huu kuna wachezaji kibao wa Man United watakuwa baba.

Siku za karibuni, Fred na kimwana wake, mrembo Monique Salum walionekana kuwa bize kufanya maandalizi ya mtoto wao wa kiume, Benjamin wakati walipomkaribisha duniani.

Supastaa, Paul Pogba amekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwa sasa chini ya kocha Solskjaer, akifunga mabao manne na kuasisti matatu kwenye kikosi hicho, naye ni mmoja wa wachezaji wanaotarajia kuitwa baba ndani ya msimu huu.

Kiungo huyo ambaye aliteseka sana chini ya Jose Mourinho, anatarajia kupata mtoto baada ya mpenzi wake, Maria Salaues kujitangaza kuwa ni mjamzito.

Mrembo huyo wa Kibolivia, Maria alikuwapo uwanjani kwenye mechi dhidi ya Huddersfield na Bournemouth na kumshuhudia baba watoto wake akifunga mabao kwenye mechi hiyo kudhihirisha kwamba staa huyo ni mkali wa mabao ya ndani na nje ya uwanja.

Beki wa kati, Victor Lindelof naye anatarajia mtoto msimu huu baada ya mkewe aliyeoana naye mwaka jana baada ya fainnali za Kombe la Dunia 2018, mrembo Maja Nilsson kutangaza kuwa naye ni mjamzito.

Mrembo Maja alijitangaza kuwa ni mjamzito kupitia ukurasa wake wa Instagram, Oktoba na huenda mtoto akazaliwa mwanzoni mwa mwezi Aprili.

Kwa sasa, Lindelof mambo yake yapo vizuri kwa sasa kutokana na kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Solskjaer.

Advertisement