Mastaa hawa pesa kiduchu tu unawanasa

Muktasari:

Kwenye usajili wa majira ya kiangazi kuna dili kibao ambazo zinaweza kufanikishwa kwa dau dogo tu kwa sababu mikataba yao inawaruhusu kuuzwa kwa bei hiyo, mfano wa dili ni hizi zifuatazo.

DORTMUND,UJERUMANI.HATA klabu kubwa duniani huwa zinahitaji wachezaji bora kwa bei ya kawaida na njia pekee ya kufanikisha hilo ni kufuatilia kwa karibu zaidi vipengele vya bei kwenye mikataba yao.

Mfano Liverpool walimnasa Takumi Minamino kutoka kwa RB Salzburg kwa Pauni 7.25 milioni tu, huku Erling Braut Haaland akiondoka kwenye klabu hiyo kwa dau la Pauni 18 milioni tu.

Kwenye usajili wa majira ya kiangazi kuna dili kibao ambazo zinaweza kufanikishwa kwa dau dogo tu kwa sababu mikataba yao inawaruhusu kuuzwa kwa bei hiyo, mfano wa dili ni hizi zifuatazo.

1. Erling Braut Haaland – Pauni 63 milioni

Kwenye ulimwengu huu wa wachezaji kuuzwa kwa bei za kutisha, Pauni 63 milioni ni dau la kawaida sana kwa mchezaji tena straika kama Haaland.

Huyu dogo alitua Borussia Dortmund kwa Pauni 18 milioni tu, lakini ni wazi kuwa wakala wake Mino Raiola alikuwa anatazama mbele zaidi na ndiyo maana akakomaa kuwepo kwa kipengele cha kuuzwa kwa dau hilo, tayari dogo huyu ana mabao manane kwenye mechi nne za Dortmund.

2. Timo Werner -Pauni 51 Milioni

Inaonekana ni jambo lisilopingika kuwa staa huyu wa Kimataifa wa Ujerumani ataondoka RB Leipzig mwisho wa msimu.

Timu yake inapigania ubingwa wa Bundesliga, lakini mwenyewe anataka kwenda kwenye klabu kubwa Ulaya.

Ana kazi kubwa na analijua goli, Liverpool na Chelsea zote kwa pamoja zimekuwa zikifukuzia saini yake. Unapotumia Pauni 51 milioni kunasa saini ya mchezaji aliyefunga mabao 20 kwenye mechi 20 ni wazi unakuwa hujapigwa.

3. Jack Grealish – Pauni 45 milioni

Katika msimu ambao Aston Villa wanapambana kutokushuka daraja, Grealish amejitengenezea jina kwa kiwango kikubwa sana katika timu ya kawaida.

Kutakuwa na klabu nyingi mwisho wa msimu ambazo zitakuwa zinataka saini yake, ukijumlisha na ukweli kuwa wachezaji wa Kiingereza huwa wanauzwa bei kubwa ni wazi kuwa kumsajili Grealish kwa Pauni 45 milioni ni bei karibu na bure.

4. Marc Roca –Pauni 33.8 milioni

Kiungo huyu alikuwa anawaniwa na Bayern Munich wakati wa usajili wa dirisha la usajili la kiangazi lililopita na kuna dalili za kumrudia tena mwisho wa msimu huu.

Thamani yake ni Pauni 33.8 milioni tu, akiwa anachezea klabu ya Espanyol ambayo iko hatarini kushuka daraja nchini Hispania ni wazi itakuwa rahisi kunasa saini yake hasa kutokana na bei na timu ambayo anachezea.

5. Unai Nunez –Pauni 25.5 milioni

Nunez ni staa mwingine kutoka Akademi ya Athletic Bilbao, tayari ameshacheza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania akifuata nyayo za Aymeric Laporte na Kepa Arrizabalaga. Ana urefu wa futi 6 na inchi 1, kama mabeki wengi wa Kihispaniola anajua kuchezea mpira na dau la Pauni 25.5 milioni lililopo kwenye mkataba wake ni la kawaida sana kwa mchezaji wa kiwango chake.

6. Lorenzo Pellegrini –Pauni 25 milioni

Kiungo huyu wa Roma ana wastani wa kupiga pasi moja ya bao kila baada ya mechi mbili na msimu huu amekuwa kwenye kiwango bora sana.

Dau la Pauni 25 milioni lililopo kwenye mkataba wake ni la kawaida sana hasa kwa mchezaji wa aina yake ambaye anaweza kucheza kama kiungo mkabaji, mshambuliaji na boksi – boksi.

7. Hwang Hee-chan – Pauni 20 milioni

Wolves walihusishwa na staa huyu wa Kimataifa wa Korea Kusini wakati wa Januari, lakini wakampotezea sasa wanaweza kumrudia wakati wa kiangazi.

RB Salzburg iliwapoteza Haaland na Minamino wakati wa Januari ndiyo maana ilikuwa ngumu kwao kumuuza wakati wa Januari, lakini kwenye kiangazi ikitokea timu ya kulipa Pauni 20 milioni. Dau ambalo la kawaida kwa mchezaji aliyefunga mabao sita na kupiga pasi za mabao saba katika mechi 14.

8. Chimy Avila – Pauni 20 Milioni

Straika huyu wa Osasuna amekuwa na kiwango bora sana msimu huu akiwa na mabao tisa kwenye mechi 20, bahati mbaya kwake atakaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuumia goti.

Lakini, dau la Pauni 20 milioni kwa straika aliyethibitisha ubora wake kwenye Ligi ngumu kama ya Hispania ni bei ya kutupa kabisa.

9. Rui Silva – Pauni 12.7 milioni

Kipa huyu wa Granada ana mchango mkubwa sana kwenye kuhakikisha timu hiyo inakuwa ngumu licha ya kupanda daraja msimu huu. Kipa huyu amecheza mechi nane bila kuruhusu bao msimu huu, kumsajili kwa Pauni 12.7 milioni ni biashara nzuri sana kwa mtu ambaye atatoa Pesa hiyo kwa Rui Silva.

10. Adolfo Gaich – Pauni 11.5 milioni

Akiwa anachezea klabu ya San Lorenzo ya kwao Argentina tayari klabu za Schalke na Villarreal zimeanza kufukuzia saini yake.

Kama Adolfo Gaich akiendelea na kasi yake hii Pauni 11.5 milioni ni kiwango kidogo sana cha pesa kulinganisha na uwezo wake pamoja na umri wake kwa sababu ndiyo kwanza ana miaka 20.