Mastaa 10 waota mbawa Man United

 MANCHESTER, ENGLAND. MASPESHALISTI wa kufeli. Ndicho unachoweza kusema kuhusu Manchester United linapokuja suala la kufanya usajili wa mastaa wapya.

Kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya lililofungwa juzi Jumatatu, kuna orodha ndefu sana ya masupastaa wa nguvu waliokuwa wakihusishwa na miamba hiyo ya Old Trafford na hadi usajili huo unafungwa, hakuna hata mchezaji mmoja aliyetajwa kwa muda wote aliyefanikiwa kunaswa na kikosi hicho kinachonolewa na Ole Gunnar Solskjaer.

Mashabiki wa Man United wanamnyooshea kidole makamu mwenyekiti Ed Woodward na kudai timu ilichokifanya ni bora usajili na sio usajili bora.

Kwenye dirisha hili, Man United imewasajili Donny van de Beek, Alex Telles, Edinson Cavani, Facundo Pellistri na kinda wa Atalanta, Amad Diallo - ambaye atatua Old Trafford Januari mwakani.

Jumapili iliyopita, kikosi hicho kilichapwa 6-1 na Tottenham Hotspur na hapo kilionekana kuwa na udhaifu kwenye beki ya kati na kiungo, lakini dirisha limefungwa hakuna usajili wa nafasi hizo uliofanyika huku Solskjaer mwenyewe ajira yake ikianza kuhusishwa na Mauricio Pochettino.

Staa wa kwanza, Jadon Sancho - ambaye kwa muda wote wa kipindi cha usajili alihusishwa na Man United, lakini miamba hiyo ilishindwa kukamilisha dili hilo kutokana na timu yake ya Borussia Dortmund kuhitaji mkwanja wa Pauni 108 milioni.

Mchezaji wa pili ni Gareth Bale. Winga huyo wa Real Madrid alikuwa tayari kabisa kwenda Man United, alipomsubiri Ed Woodward kwa muda mrefu, hakutokea aliamua kutimkia zake Spurs kwenye timu yake ya zamani alikojiunga kwa mkopo.

Staa wa tatu ni Sergio Reguilon, Man United walimsaka sana, lakini walijichelewesha na matokeo yake akanaswa na Spurs. Man United ikakosa huduma yake.

Wa nne ni Federico Chiesa. Mwanzoni tu mwa dirisha la usajili, Man United ilionyesha dhamira ya kunasa saini yake, lakini kama kawaida walijichelewesha na matokeo yake akanaswa na Juventus. Beki wa kushoto, Ben Chilwell lilikuwa chaguo la kwanza la Man United kwa wachezaji wa namba hiyo waliokuwa ikiwasaka, lakini Chelsea ikamnasa.

Mchezaji wa sita ni Jack Grealish. Staa huyo Mwingereza tangu mwanzoni kabisa mwa dirisha la usajili na wengi waliamini mkali huyo wa Aston Villa atakwenda Old Trafford. Man United hawakueleweka na Grealish alisaini dili jipya la kuendelea kubaki Villa Park. Mchezaji wa saba ni James Maddison wa Leicester City na ilionekana kama vile angetua Man United, lakini naye aliwaona wababe hao wa Old Trafford hawapo siriazi kwenye mipango yao ya usajili na kuamua zake kusaini dili jipya huko King Power na atakaa hadi 2023.

Mchezaji wa nane ni beki wa kati, Kalidou Koulibaly. Wengi waliamini Koulibaly atakwenda Old Trafford kucheza sambamba na Harry Maguire, hasa kwa kipindi hiki safu ya beki ya miamba hiyo kuonekana kuwa na matatizo makubwa. Dili hilo pia halikukamilika.

Man United ikahamia kwa Ismaila Sarr. Kila kitu kilionekana kama vile kinda huyo wa Watford angetua huko Old Trafford, lakini hadi dirisha linafungwa, Sarr alikuwa mchezaji wa tisa, ambaye ametajwa na kuhusishwa sana na Man United hakunaswa na miamba hiyo.

Staa wa 10 ni Ousmane Dembele. Hadi kufikia siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, fowadi huyo wa Barcelona alihusishwa na Man United angenaswa na miamba hiyo ya Old Trafford. Lakini, ilishindwa kukamilisha dili hilo kwa wakati na licha ya kudaiwa ilipeleka Nou Camp ofa ya Pauni 55 milioni kwa ajili ya kunasa huduma ya Dembele dakika za mwisho, Barcelona iligoma kufanya biashara kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili kwa sababu na wao hawakuwa wamekamilisha dili la Memphis Depay.