Masoud kuikamua Simba mamilioni

Muktasari:

  • Kitendo cha kocha msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma kufutwa kazi ndani ya kikosi hicho kitamfanya aondoke nchini mfuko ukiwa umenona, kutokana na pesa za malipo juu ya kuvunjwa kwa mkataba wake.

MABOSI wa Simba wamekubaliana kuachana na kocha msaidizi wao, Masoud Djuma, lakini kocha huyo kutoka Burundi anatarajia kuivuna klabu hiyo fedha za maana ikiwa ni fidia ya kuvunjwa mkataba wake.

Masoud alitua Simba na kutambulishwa rasmi Oktoba 19, mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili, lakini hadi anasitishiwa mkataba huo tayari alishautumikia mwaka mmoja na hivyo mabosi wa Msimbazi wanapaswa kumlipa chake kabla ya kusepa zake.

Kocha huyo aliyekuwa akidaiwa huenda angeondoka jana Jumapili, imeelezwa amegoma kutimka mpaka apewe chake, huku ikielezwa kuwa wakati akiitumia Simba alikuwa akilipwa Dola 2,500 (zaidi ya Sh5 milioni) kwa mwezi.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliliambia Mwanaspoti jana Jumapili kuwa, baada ya kuvunja mkataba wake ulikuwa unaonesha kama Simba itavunja mkataba itatakiwa kulipa mshahara wa mwezi mmoja na stahiki zake nyingine ikiwamo tiketi ya ndege.

Mkataba wa Djuma unaonesha kama Simba itauvunja kama ilivyofanya itatakiwa kulipa mshahara wa mwezi mmoja ili kila upande kuendelea na majukumu yake.

Kwa maana hiyo, Djuma atalipwa Sh 5 milioni kama mkataba wake unavyosema pindi ukivunjwa na Simba na fedha nyingine zitatokana na bonansi kulingana na timu ilivyofanya vizuri sambamba na kumsafirisha kumrudisha kwao.

“Tutampa bonansi zake zote na hiyo Sh 5 milioni ambayo ipo katika kipengele cha kuvunja mkataba na baada ya kukamilisha hayo tutampa tiketi ya ndege ya kwenda kwako,” alisema kigogo huyo ambaye hakutaka kutwajwa jina lake hadharani.

Hata hivyo, kuvunjwa kwa mkataba wa Djuma kumekuwa tofauti na ilivyokuwa kwa Jackson Mayanja aliyerithiwa na Mrundi huyo, kwani Simba ililazimika kulipa mishahara ya miezi mitatu na kubeba kitita kirefu kama ilivyokuwa kwa bosi wake Joseph Omog.

Fununu zinadai Djuma bado anatakiwa na baadhi ya timu za Ligi Kuu nchini.