Mashujaa wapania kuifuata Simba juu

Friday July 12 2019

 

By Masous Masasi


BAADA ya mabosi wa Mashujaa FC kumwongezea mkataba Kocha Atuga Manyundo, ametamka kuwa anataka msimu ujao wa Ligi Daraja la Kwanza arudishe heshima ya Mkoa wa Kigoma kwa kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo.

Kocha huyo aliisaidia timu hiyo isishuke daraja msimu uliopita na pia aliiwezesha kuifunga Simba mabao 3-2 katika mchezo wa Kombe la FA.

Akizungumza na Mwanaspoti, Manyundo alisema baada ya kukabidhiwa timu mipango yake ni kurejesha heshima ya soka la Kigoma kwa kuipandisha Ligi Kuu.

Alisema msimu uliopita alishindwa kuipandisha timu hiyo kwani alikabidhiwa katika mzunguko wa pili ambapo kitu alichokifanya ni kuhakikisha haishuki daraja kwa kuwa aliikuta inavuta mkia kwenye msimamo.

“Nina jukumu zito la kurejesha hadhi ya Mkoa wa Kigoma, ni miaka tarkibani 20 sasa hawana timu ya ligi, hivyo ni jukumu langu kuhakikisha tunaipa heshima uliojiwekea kipindi cha nyuma,” alisema Manyundo.

Alisema kuanzia keshokutwa Jumamosi wataanza usajili ambapo anataka kikosi chake kiwe na wachezaji 23 wapambanaji ambao wataipa mafanikio klabu hiyo.

Advertisement

“Tuko katika mazunguko na wachezaji mbalimbali kwani nitaongeza saba pekee huku 16 tutawaongezea mkataba. Nitaongeza kipa, beki na kiungo,” alisema.

Advertisement