Mashindano ya riadha Taifa yaota mbawa tena

Muktasari:

Kalenda ya RT mashindano hayo yalipangwa kufanyika Mei na Juni, lakini yakapigwa kalenda hadi Agosti na kisha Novemba yameahirishwa tena.

Dar es Salaam. Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), limethibitisha rasmi kuahirishwa kwa mashindano ya Taifa yaliyokuwa yafanyike Ijumaa na Jumamosi jijini Dar es Salaam.

RT haijaweka wazi tarehe rasmi ya mashindano hayo ingawa imesisitiza yatafanyika mwaka huu.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelim Gidabuday alisema yatafanyika baada ya Mashindano ya Wanawake ya ‘JICA First Lady’ ya Novemba 24 na 25.

"Tarehe mpya ya mashindano ya Taifa itatangazwa baadae, mikoa iendelee na mazoezi, kwani ni lazima Mashindano ya Taifa kufanyika mwaka huu," alisema.

Japo hakuweka wazi sababu ya kuahirishwa mashindano hayo, lakini habari za ndani zinasema ni kutokana na kukosa fedha.

Mwaka jana RT ilishindwa kuandaa mashindano ya Taifa kitendo kilichowaweka kwenye mazingira magumu na kunusurika kunyimwa fedha za IAAF za kila mwaka dola 10,000.