Mashabiki Yanga wamshangaa mwamuzi

Muktasari:

Baada ya mpira kumalizika mashabiki hao walitoka nje ya Uwanja na kujikusanya  vikundi vikundi huku wakijadili kipigo hicho na wengine wakianza kumrushia maneno mwamuzi wa mchezo huo George Gatogato kutoka Burundi kuwa amesababisha wafungwe.

Dar es Salaam.Ukitaka kuona hasira za mashabiki wa Yanga,basi timu yao ifungwe na si kufungwa tu bali ifungwe huku wakiamini  wameonewa.
Ndicho kilichojiri baada ya mchezo wa kombe la SportPesa baada ya Yanga kukubali kipigo cha mabao 3-2  kutoka kwa Kariobangi Sharks ya Kenya.
Baada ya mpira kumalizika mashabiki hao walitoka nje ya Uwanja na kujikusanya  vikundi vikundi huku wakijadili kipigo hicho na wengine wakianza kumrushia maneno mwamuzi wa mchezo huo George Gatogato kutoka Burundi kuwa amesababisha wafungwe.
Mashabiki wengine walimlaumu kocha Mwinyi Zahera kuwa alikosea kupanga timu huku wengi  wakimtetea kuwa kocha huyo Wala hana makosa kwani  kikosi ni kile kile cha kila siku.
Bao la tatu la Kariobangi lililofungwa na Abuya Duke ndilo lililoleta kizaazaa uwanjani hapo baada ya kudaiwa kuwa bao hilo lilifungwa wakati kiungo wa Yanga Papy Kabamba Tshishimbi akiwa chini baada ya kufanyiwa  madhambi.
Wakati mwamuzi akilikubali bao hilo wachezaji wa Kariobangi walikwenda upande wa mashabiki wa Yanga na kushangilia kwa kuwakejeli na mashabiki hao kujibu mapigo kwa kuwarushia chupa za maji.