Mashabiki Singida United waisikilizia Yanga

Muktasari:

Viingilio vya mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 10 jioni, jukwaa kuu ni Sh10,000 wakati majukwaa mengine yote ya kawaida ni Sh.5,000.

 

Singida. Imezoeleka nyakati zote siku timu mbili kubwa nchini, Simba au Yanga zinapokuwa na mchezo sehemu husika huwa na shamrashamra nyingi.
Achana na zinapocheza jijini Dar es Salaam,purukushani zaidi hujitokeza pindi timu hizo zinapokwenda kucheza mikoani hali ya miji husika huchangamka kwa kiasi kikubwa.
Simba au Yanga zinapokuwa na mechi zao katika viwanja vya mikoa husika kuanzia asubuhi ni kawaida watu kukusanyika makundi makundi na kufurika nje ya uwanja utakaotumiwa kuchezwa mchezo huo.
Kwa hali ilivyo ambayo ni tofauti na kawaida,leo mjini Singida ni kama kuna mchezo wa timu ya Singida United dhidi ya timu nyingine za ligi kuu ambazo sio Yanga na Simba.
Mwanaspoti ambalo limepita mitaa tofauti mjini hapa ikiwemo sokoni na stendi ya mabasi Misuna haijakutana na shamrashamra kubwa wala tofauti yoyote kubwa zaidi ya utulivu na watu wakiendelea na shughuli zao.
Licha ya geti kuu la uwanja wa Namfua kuruhusu watu kuanza kuingia uwanjani kama ilivyotarajiwa saa 5 asubuhi hali ni tofauti.
Nje ya uwanja hakuna watu kama ilivyotarajiwa na waliokuwepo kwa uchache wao nao hawajaanza kuingia zaidi ya baadhi yao kuondoka eneo hilo.
Inawezekana mchezo huo unachezwa siku ya kazi hata hivyo hiyo haijawa sababu ya baadhi ya watu wakiwemo wasimamizi wa mchezo na getini kushangazwa na hali hiyo kulingana na ukubwa wa timu ya Yanga nchini.