Mashabiki Al Masry wapigwa ‘stop’ kuiona Malindi

Thursday September 12 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Shirikisho la soka Misri (EFA), limewaambia Al Masry mchezo wake wa marudiano wa kombe la shirikisho Afrika dhidi ya Malindi ya Tanzania utacheza bila ya mashabiki kutokana na sababu za kiusalama.

Tamko hilo la EFA limetolewa kufuatia vurugu za hapa na pale ambazo zimekuwa zikitokea nchini humo katika michezo mbalimbali ya ushindani hivyo hili inaweza kuwa na faida kwa Malindi watakaokuwa ugenini Septemba 27.

Malindi wanatakiwa kutumia vizuri mchezo wao wa nyumbani Jumapili ili kwenda kumalizana na Waarabu hao nchini kwao ambako hawatakumbana na presha kutoka kwa mashabiki.

Mara kadhaa timu za Tanzania zimekuwa zikikutana na presha kutoka kwa mashabiki wa timu za Uarabuni kutokana na tabia ya kuzishangilia muda wote timu zao pindi zinapocheza.

Malindi walitinga raundi ya kwanza ya kombe la shirikisho baada ya kuing’oa Mogadishu City ya Somalia kwa jumla ya matokeo ya bao 1-0 ambalo walilipata kwenye mchezo wa marudiano visiwani, Zanzibar, Agosti 24.

Kikosi cha Al Masry kinachotarajiwa kuhusika na mchezo wa kwanza dhidi ya Malindi kwa mujibu wa taarifa kutoka Misri kinawachezaji 23 ambao ni makipa: Ahmed Masoud, Ahmed Abdelfatah, Mohamed Shehata.Mabeki: Karim El-Eraky, Islam Abou-Slima, Ahmed Shousha, Mahmoud Hamad, Abdelnasser Di Maria, Omar Kamal.

Advertisement

Viungo: Farid Shawky, Haggag Oweis, Amr Mousa, Ahmed Yasser, Meftah Taqtaq, Cheick Moukoro, Eze Emeka, Islam Ateya, Hassan Ali, Saïdou Simporé, Hussein Ragab. Washambuliaji: Ahmed Gomaa, Mahmoud Wadi, Austin Amutu.

Advertisement