Mashabiki 120 waishuhudia KMC ikipigishwa kwata

Muktasari:

Katika jukwaa la mzunguko walionekana kuwepo mashabiki wasiopungua 80, waliokuwa wamekaa jukwaa hilo ambao kila mmoja alilipa kiingilio cha Sh 5000.

LIGI Kuu Bara inaendelea leo Jumamosi kwenye viwanja mbalimbali huku Dar es Salaam, kukiwa na mechi tatu zinazoendelea kuchezwa.

Mechi ya kwanza ilichezwa saa 8, mchana Uwanja wa Uhuru ambayo iliwakutanisha KMC dhidi ya Polisi Tanzania.

Katika mechi hiyo kabla ya dakika chache kumalizika MCL Online lilifanya tathimini kwa mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kushuhudia pambano hilo.

Katika jukwaa la mzunguko walionekana kuwepo mashabiki wasiopungua 80, waliokuwa wamekaa jukwaa hilo ambao kila mmoja alilipa kiingilio cha Sh 5000.

Jukwaa kuu (VIP), ukiachana na viongozi pamoja na Waandishi wa Habari, mashabiki walionekana kutopungua 30 ambao kila mmoja alilipa Sh 10000.

Mechi ilivyokuwa
Ukiachana na idadi hiyo ya mashabiki waliojitokeza mechi hiyo ilimalizika kwa KMC kufungwa mabao 3-2.

Polisi Tanzania ndio walikuwa wa kwanza kupata mabao 2-0, kipindi cha kwanza yaliyofungwa Marcel Kaheza pamoja na Matheo Anthon.

KMC walirudi kipindi cha pili kwa kufanya mashambulizi hatari na kupata mabao mawili ya kusawazisha yaliyofungwa na Abdul Hilal kwa penati na Ally Ramadhani 'Oviedo'.

Baada ya kupata mabao hayo mawili ya kusawazisha KMC, walionekana kupoteza umakini hasa safu ya ulinzi iliyosababisha wapinzani wao kufunga bao la tatu na ushindi kupitia Baraka Majogoro dakika chache kabla ya mchezo kumalizika.