Mapacha watatu hatari wanapolisogelea goli

Muktasari:

  • Hawa hapa mapacha watatu waliotisha kwenye kupasia nyavu kwenye Ligi Kuu bora kabisa za huko Ulaya kwa msimu uliomalizika hivi karibuni. Ukiona wapo kwenye timu, wameanzishwa pamoja, basi ujue nyavu zitateseka siku hiyo.

LONDON, ENGLAND.UTATU wa mauaji kwenye soka. Siku hizi mpira umebadilika sana, ambapo timu zimekuwa zikitegemea mfumo wa kutumia watu watatu kwenye fowadi zao ili kufunga mabao ya kutosha kupata ushindi.

Kwa utamaduni huo kuna baadhi ya timu zimekuwa zikivuna mabao mengi, yakifungwa na mchezaji mmoja mmoja na mengine yakihusisha timu nzima.

Kwenye mfumo huo wa kutumia washambuliaji kufunga mabao, kuna baadhi ya timu zimevuna mambo mengi sana kutokana na safu yake ya ushambuliaji kuwa bize kwenye kusukumia mipira tu nyavuni na kuzifanya timu zao kushinda mechi.

Hawa hapa mapacha watatu waliotisha kwenye kupasia nyavu kwenye Ligi Kuu bora kabisa za huko Ulaya kwa msimu uliomalizika hivi karibuni. Ukiona wapo kwenye timu, wameanzishwa pamoja, basi ujue nyavu zitateseka siku hiyo.

7. Pogba – Lukaku – Rashford (mabao 35)

Manchester United haikuwa na maajabu kwa msimu uliopita na ndiyo maana ilimaliza katika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England na hivyo kujikuta ikishindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Lakini kikosi hicho cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer safu yake ya ushambuliaji iliyokuwa na wakali kama Paul Pogba, Romelu Lukaku na Marcus Rashford ilihusika kwenye mabao 35 kwenye ligi hiyo.

Pogba alifunga 13, Lukaku 12 na Rashford 10 na kufanya kuwa moja kati ya timu iliyokuwa na fowadi ya wakali watatu hatari kwa kutupia mipira kwenye nyavu za wapinzani.

Hata hivyo, haifahamiki kama fowadi hiyo ya wakali hao watatu itakuwa hivyo tena msimu ujao kutokana na Lukaku kutakiwa Inter Milan na Pogba anawindwa na Real Madrid.

6. Milik – Mertens – Insigne (mabao 43)

Huko kwenye Serie A, Napoli ilikuwa moto kabisa na kuonyesha upinzani mkali kwenye mbio za ubingwa, ambapo Juventus waliibuka wababe kwa msimu wa nane mfululizo.

Napoli ilikuwa ikijivunia safu yake hatari ya washambuliaji watatu ilikuwa inafanya jambo moja tu kwa ufasaha, kuweka mpira kwenye nyavu. Wakali watatu wanaounda fowadi hiyo ni Arkadiusz Milik, Dries Mertens na Lorenzo Insigne, ambao kwa pamoja wamehusika kwenye mabao 43.

Milik amefunga mara 17, Mertes mabao 16 na staa Insigne ameweka kwenye nyavu za wapinzani mara 10 katika Serie A msimu uliomalizika.

Kwa misimu kadhaa sasa Napoli imekuwa ikishindwa kuipoka ubingwa Juventus licha ya kuanza ligi vizuri na kushindwa kumalizia mwishoni.

5. Alcacer – Reus – Sancho (mabao 47)

Borussia Dortmund itakuwa inajishangaa yenyewe ilikosea wapi na kushindwa kumaliza utawala wa Bayern Munich kwenye Bundesliga msimu huu. Imeshindwa kubeba ubingwa huo ikizidiwa pointi mbili tu licha ya kuongeza ligi kwa muda mrefu hadi hapo iliposhushwa kileleni kwenye wiki tatu za mwisho za kumaliza msimu.

Kikosi chake kimefunga mabao ya kutosha na kuwa timu inayoshika namba tano kwenye ligi za Ulaya kuwa na safu ya washambuliaji watatu iliyokuwa kiboko kwa kufunga mabao, Paco Alacer alifunga 18, Marco Reus 17 na Jadon Sancho 12, kuifanya ifunge jumla mabao 47 kwenye ligi.

Staa Sancho amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali na kama atahama, basi Dortmund itakuwa na kazi ya kumtafuta mbadala wake.

4. Aguero – Sterling – Sane (mabao 48)

Manchester City ilimaliza msimu kwa kubeba mataji yote matatu ya ndani ya England ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu England, ambapo washambuliaji wake walikuwa moto kwelikweli kwa kufunga mabao.

Kikosi hicho cha Etihad kinachonolewa na Mhispaniola, Pep Guardiola kilijivunia kuwa na safu moto ya washambuliaji watatu iliyoundwa na Sergio Aguero, Raheem Sterling na Leroy Sane, ambao wamehusika kwenye mabao 48 kwenye ligi. Safu hiyo ya kombinesheni ya fowadi watatu, Aguero amefunga mabaoa 21, Sterling ameweka wavuni mara 17 na Sane amefunga mara 10.

Fowadi hiyo ndiyo iliyoibeba Man City na kutamba kwenye Ligi Kuu England ikibeba ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo. Sane anahusishwa na mpango wa kuondoka kwenye timu hiyo ambapo Bayern Munich inapiga hesabu za kuinasa saini yake.

3. Salah – Mane – Firmino (mabao 56)

Liverpool ilitoka kapa kwenye Ligi Kuu England ikishindwa kubeba taji hilo kwa tofauti ya pointi moja tu iliyozidiwa na Manchester City. Lakini wababe hao wa Anfield wamekwenda kumaliza machungu yao ya kushindwa kubeba taji la ligi kwa kunyakua ubingwa wa Ulaya, walipoichapa Tottenham kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kubeba taji lao la sita.

Hata hivyo, kukosa kwao ubingwa wa ligi haukusababishwa na kukosekana kwa mabao, kwa sababu walikuwa na safu hatari ya washambuliaji watatu ambao wenyewe walikuwa bize kutupia mipira nyavuni.

Fowadi hao, Mohamed Salah na Sadio Mane kila mmoja alifunga mara 22 wakati pacha wao Roberto Firmino yeye alitikisa nyavu mara 12 na kufanya wawe wamehusika kwenye mabao 56. Kocha Jurgen Klopp ana uhakika wa kubaki na fowadi yake hiyo.

2. Messi – Suarez – Dembele (mabao 65)

Barcelona imebeba ubingwa wake wa La Liga kirahisi tu katika msimu wa pili mfululizo, ikibeba baada ya kuweka pengo la pointi 11 kileleni dhidi ya timu iliyoshika nafasi ya pili, Atletico Madrid. Kutokana na wepesi huo wa Barcelona kwenye kubeba ubingwa, imekuwa salama kwenye mikono ya supastaa wake wa Kiargentina, Lionel Messi, ambaye ndiye aliyebuka kinara wa mabao kwenye La Liga msimu huu akiwa ameweka wavuni mara 36.

Kwenye fowadi ya Barca ya wakali watatu, Messi anashikiliana vyema kabisa na Luis Suarez, aliyefunga mabao 21 na Ousmane Dembele mabao manane na kufanya kuwa na idadi ya mabao 65.

Ukiweka kando mabao, wakali hao watatu wametengeneza pia pasi za mabao kwa wenzao, Messi akiasisti mara 13, Suarez sita na Dembele asisti tano. Msimu ujao fowadi hiyo inaweza kubadilika kama Barca itawanasa Antoine Griezmann au Alexandre Lacazette inazifukuzia saini zao.

1. Cavani – Mbappe – Neymar (mabao 66)

Paris Saint-Germain ni wababe wengine wa ligi bora za Ulaya ambao walibeba ubingwa kirahisi sana msimu huu. Wakati hao wa Ufaransa walinyakua taji la Ligue 1 kibabe na hivyo kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao wakiwa na hamu ya kufanya vizuri zaidi baada ya kuchemka kwa miaka ya karibuni.

Kwa sababu Neymar na Edinson Cavani walikuwa majeruhi na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, pacha wao Kylian Mbappe aliendelea kutamba uwanjani na kumaliza msimu akiwa amefunga mabao 33 kwenye ligi hiyo.

Lakini wakali wengine Neymar alifunga mara 18 na Cavani mara 15 na hivyo kufanya safu hiyo ya wakali watatu kufunga mabao 66. PSG sasa itabidi itafute pacha mwingine wa Neymar na Mbappe kutokana na ripoti zinazodai Cavani anapiga hesabu za kuhama.