Manula apata ahueni Afcon

Tuesday June 11 2019

 

By Charles Abel

WASHAMBULIAJI wawili ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kumtungua kipa Aishi Manula, watakosekana kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu baada ya kuenguliwa kwenye vikosi vya mwisho vya wachezaji 23 vya mataifa yao.

Nyota hao ni mshambuliaji wa Nigeria anayechezea Leicester City ya England, Kelechi Iheanacho na nyota wa DR Congo, Jackson Muleka ambaye anaitumikia TP Mazembe.

Iheanacho ambaye aliwahi kumtungua Manula katika mechi ya kuwania kufuzu Afcon mwaka 2017 ambao ulichezwa dimba la Akwa Ibom ameshindwa kingia kikosi cha nyota 23 wa Nigeria ‘Super Eagles’ ambacho kitashiriki AFCON baada ya kupigwa chini na Kocha Genort Rohr ambaye hajaridhishwa na kiwango chake.

Kwa upande wa Muleka ambaye alifunga bao la ushindi wakati Mazembe ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Simba kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Stade De Mazembe, naye ameondolewa kwenye kikosi cha DR Congo kutokana na masuala ya uhamiaji.

Kuchelewa kupata vibali vya kuingia Hispania ambako DR Congo imeweka kambi yake ya maandalizi, kumelifanya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Florent Ibenge kumwengua mshambuliaji huyo pamoja na mwenzake Kabango Kasongo anayechezea Al-Wahda

Ukiondoa Iheanacho na Muleka, staa mwingine ambaye atazikosa fainali hizo ni Sam Ajayi ambaye naye ameenguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa Nigeria.

Advertisement

Advertisement