Manula afunika kwa ubora makipa AFCON

Wednesday June 26 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam.Raundi ya Kwanza ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea huko Misri imekamilika rasmi jana kwa mechi zilizokutanisha Ghana dhidi ya Benin na ile ya Cameroon dhidi ya Guinea-Bissau na leo hatua ya pili itaanza kwa mechi tatu ambazo zitakutanisha wenyeji Misri dhidi ya DR Congo, Uganda dhidi ya Zimbabwe na mechi nyingine itakuwa baina ya Nigeria na Guinea.

Ushindani wa hali ya juu umeonekana kwenye mechi za raundi ya kwanza za makundi sita ya mashindano hayo, wapo waliokenua meno kwa kupata ushindi, kuna waliotoka sare lakini pia wapo waliolia kwa kupoteza mechi zao za kwanza.

Wapo nyota waliochemsha pia baadhi yao wameonyesha kiwango bora kwenye mechi hizo za kwanza ambacho pengine kinaweza kuwa neema kwao ya kutazamwa kwa jicho la tatu kwenye fainali hizo na labda kuwa daraja kwao kupata malisho ya kijani kwenye klabu mbalimbali duniani.

Katika kundi hilo la nyota waliofanya vizuri, wale wanaocheza nafasi ya kipa ndio wameonekana kutamba zaidi kwenye mechi za mwanzo za hatua ya makundi na makala hii inatoa tathmini ya mfano wa makipa ambao kiwango chao, kinatoa ishara njema kuwa huenda safari hii wachezaji wanaocheza nafasi hiyo ndio wakateka mashindano hayo.

Aishi Manula-Taifa Stars

Pamoja na Taifa Stars kufungwa mabao 2-0 na Senegal, hakuna namna ambayo Watanzania wanaweza kukwepa kumshukuru kipa Aishi Manula kwani kama asingeonyesha kiwango bora kwenye mchezo huo pengine Tanzania ingeadhirika kwa kutandikwa idadi kubwa ya mabao.

Advertisement

Takwimu za mechi hiyo zinaonyesha kuwa Senegal walipiga mashuti 13 yaliyolenga lango na kati ya hayo Manula aliokoa nane (8) ambayo kwa kipa wa daraja la kawaida, yote yangejaa kimiani.

Edmore Sibanda-Zimbabwe

Kuna usemi unasema kuwa 'Kipa ni kama mvinyo' ukimaanisha kuwa kadri umri wa kipa unavyoongezeka ndivyo ubora wake unavyoimarika zaidi.

Unaweza kutumia kauli hiyo kuelezea ubora wa kipa Edmore Sibanda wa Zimbabwe ambaye katika umri wa miaka 32 amekuwa tegemeo la timu hiyo kwenye fainali za AFCON.

Kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Misri, licha ya kuruhusu bao moja, Sibanda aliwanyima wenyeji nafasi nane (8) za wazi za mabao kutokana na ustadi wake wa kuokoa michomo na pengine kipa huyo anayedakia Witbank Spurs FC ya Afrika Kusini, Zimbabwe ingepokea kipigo cha aibu.

Loydt Kazapua-Namibia

Kila mmoja alitegemea kuona Namibia ikipokea kipigo cha mbwa mwizi kutoka kwa wababe Morocoo kwenye mechi baina yao iliyochezwa Juni 23 kutokana na utofauti mkubwa wa ubora uliopo baina ya timu hizo mbili.

Hata hivyo pamoja na Morocco kutawala dakika zote za mchezo na kuishambulia kama nyuki, Namibia ikipiga jumla ya mashuti tisa yaliyolenga lango, ilijikuta ikipata ushindi kiduchu wa bao 1-0.

Matokeo hayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na kiwango bora cha kipa wa Namibia, Loydt Kazapua ambaye katika mashuti tisa aliyopigiwa, aliokoa matano (5) ya ana kwa ana.

Jonas Mendes-Guinea Bissau

Cameroon walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Guinea Bissau kwenye mchezo wao wa kwanza uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Ismailia huko jijini Ismailia.

Mabingwa hao watetezi wangeweza kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 lakini uhodari wa kia Jonas Mendes wa Guinea Bissau ambaye aliokoa mashuti matatu ya ana kwa ana ambayo yaliinyima nafasi Cameroon kupata ushindi mkubwa kwenye mechi hiyo.

Brahim Souleimane-Mauritania

Mauritania ilianza vibaya kwa kuchapwa mabao 4-1 lakini bado wanastahili kumshukuru kipa wao Brahim Souleimane mwenye umri wa miaka 32 ambaye kwenye mechi hiyo aliokoa michomo mitano ya wazi kutoka kwa washambuliaji wa Mali ambayo kama ingejaa nyavuni maana yake timu yake ingemaliza mechi ikiwa imefungwa mabao 9-1.

Advertisement