Mane, Salah wampa homa klopp

Muktasari:

Kipa Alisson Becker pia yuko mapumziko baada ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Brazili katika michuano ya Copa America sawa na Firmino wakati Salah na Mane walikuwa kwenye AFCON Misri.

LIVERPOOL, ENGLAND.LIVERPOOL imeshaanza kujifua kwa ajili ya msimu mpya huko, lakini presha imempanda Kocha Jurgen Klopp kuhusu uchovu wa nyota wake.

Wakati wakali kibao wamesharejea kambini, bado mastaa kadhaa hawajarudi wakiwamo wale ‘watu wabaya’ wote watatu wa safu yake ya ushambuliaji – Roberto Firmino, Mohamed Salah na Sadio Mane.

Kipa Alisson Becker pia yuko mapumziko baada ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Brazili katika michuano ya Copa America sawa na Firmino wakati Salah na Mane walikuwa kwenye AFCON Misri.

Huku msimu mpya ukianza ndani ya siku 15 zijazo kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Liverpool na Manchester City Agosti 4, Klopp presha inampanda.

“Huu ni msimu wa miezi 13,” alisema Klopp, akikiri ‘hofu’ yake kutokana na uchovu wa wachezaji wake ambao wanalazimika kucheza miezi mingi bila ya kupata mazumziko ya kutosha.

“Sitaki kuonekana kama nalialia, lakini hii iko wazi kabisa.

“Tunapaswa kuona tutakabiliana vipi na hali hii. Wabrazili wamemaliza msimu vizuri wakishinda mataji mawili, kwa Mo ni tofauti lakini tunawasiliana mara kwa mara na wote watatu wako poa.

“Suala la Sadio ni spesho kwa sababu michuano hii imechukua muda mrefu na zimebaki siku chache tuikabili Man City. Nitazungumza naye haraka baada ya mechi yao (ya fainali ya AFCON baina ya Senegal na Algeria jana usiku) na tutaona inakuwaje.”