Manchester United yampa mkono wa kwakheri Bale

Thursday June 13 2019

 

Manchester, England. Ndoto za nyota wa Real Madrid, Gareth Bale kujiunga na Manchester United katika kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili zimegonga mwamba baada ya klabu hiyo kumuondoa katika orodha ya wachezaji walio kwenye mpango wa kuwasajili.

Bale (29) ameshaonyeshwa mlango wa kutokea na kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amemueleza wazi kuwa hana mpango naye na ilionekana kuwa angetimkia United ambayo imekuwa ikimtamani kwa muda mrefu.

Hata hivyo imedaiwa kuwa Kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer amepanga kujenga timu mpya kwa kusajili idadi kubwa ya wachezaji vijana na hivyo Bale hayupo kwenye mipango yake.

Tayari Solskjaer ameshaanza kutimiza kwa vitendo mpango wake wa kuijenga United kupitia damu changa baada ya hivi karibuni kumnasa winga wa Wales, Daniel James kwa ada ya Pauni 17 milioni kutoka Swansea.

Uamuzi huo unaweza kuwa muendelezo wa mapigo ambayo Bale amekuwa akiyapata katika kikosi cha Real Madrid katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo hasa chini ya utawala wa Zidane.

Maisha ya Bale yanazidi kuwa magumu zaidi baada ya Real Madrid kumsajili nyota wa Chelsea, Eden Hazard pamoja na mshambuliaji wa Entracht Frankfurt, Luka Jovic.

Advertisement

Advertisement