Manara: Hakuna mwenye nguvu Simba

Muktasari:

Washabiki wa Simba wamekuwa na tabia ya kufanya vurugu kila timu yao inapopata matokeo vibaya

Shinyanga. Afisa Habari wa Simba, Haji Manara ameibuka na kuvunja ukimya kutokana na kitendo cha mashabiki kufanya vurugu timu yao inapopoteza mechi kwamba kitendo hicho ni cha kihuni.
Wiki iliyopita mashabiki wa Simba walimrushia chupa za maji kocha Patrick Aussems baada ya timu yao kupoteza mechi dhidi ya Mbao iliyochezwa uwanja wa Kirumba jijini Mwanza
Mbali na kocha kurushiwa chupa za maji pia Manara alirushiwa chupa ya maji lakini amesema kwake huwa hajali kuliko kitendo wanachomfanyia Mbelgiji wao.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa uwanja wa Kambarage na kupata ushindi wa mabao 3-1, Manara alisema hakufurahishwa na kitendo hicho.
"Nani ama timu gani haijawahi kufungwa ama kutoka sare, leo hii mashabiki wanamtupia chupa za maji kocha kwa kosa gani alilofanya, hizi ni tabia za wapi inakera na kuumiza hivi tutapata kweli makocha bora wa kuja hapa kufundisha kwa mfumo huu wa kuwarushia chupa.
"Inafikia kipindi unatamani hata kuachana na mambo ya mpira lakini wakumbuke kwamba Simba si ya mtu mmoja na hakuna aliyejuu ya Simba, kwani kila mtu ndani ya Simba anapita, siyo mimi, siyo kocha wala mtu mwingine yoyote.
"Kuna mambo mengi hawayaelewi ndiyo maana wanapiga kelele kila wanapotumiana ujumbe ama kujadili kwenye makundi yao,  mashabiki wanapaswa tubadilike, tulipoteza Mwanza, lakini huku tumeshinda huo ndiyo mpira, nashukuru wachezaji wanampa sapoti mwalimu wao," alisema Manara ambaye alikuja uwanjani kuishuhudia timu yake japo akiwa anaumwa.
Simba walirejea jijini Dar es Salaam jana Jumatatu jioni ambao ilidaiwa kuwa leo Jumanne watakwenda kupiga kambi kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Yanga itakayochezwa wikiendi hii.