Man United hadi aibu, penalti nyingii hadi wamepenya Ulaya

Tuesday July 28 2020

 

HUKO uswahilini, Manchester United imekuwa gumzo, kwamba imebebwa kukamatia tiketi yao ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Mashabiki wapinzani wa miamba hiyo ya Old Trafford, wanaita Man United “Mama Nibebe” baada ya waamuzi kuwapa penalti nyingi msimu huu, ikiwamo kwenye mechi yao ya mwisho kwenye Ligi Kuu England, ambayo ilitoa hatima yao ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Juzi Jumapili, Man United ilikuwa ugenini King Power kukabiliana na Leicester City, ambao pia walikuwa wakipambania nafasi kwenye Top Four ili kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini penalti moja tu ilibadili kila kitu.

Katika mchezo huo wa juzi, ambapo Man United ilishinda 2-0, bao lao la kwanza lilikuwa la penalti baada ya mwamuzi Martin Atkinson kuwapa vijana wa Ole Gunnar Solskjaer penalti ya 14 ndani ya msimu huu.

Kwa rekodi hiyo, Man United ndiyo timu iliyopewa penalti nyingi kuliko timu nyingine yoyote kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Penalti 14.

Kiungo mchezeshaji, fundi wa mpira Bruno Fernandes alifunga penalti hiyo, iliyotokana na staa wa zamani wa Man United, beki Jonny Evans na veterani wa Foxes, Wes Morgan kumwangusha Anthony Martial ndani ya boksi, wakati alipokuwa akikimbia kuelekea golini.

Advertisement

Penalti hiyo imewafanya Man United kuwa timu iliyopewa mikwaju mingi kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu na hivyo kuandika rekodi mpya kwenye mikikimikiki hiyo.

Jambo hilo limewafanya kuvunja rekodi ya Crystal Palace katika msimu wa 2004-05 na Leicester City katika msimu ambao walibeba ubingwa wa Ligi Kuu England, 2015-16, ambapo timu hizo zilipewa penalti 13 kila moja ndani ya msimu mmoja.

Katika msimu wa 2009-10, kocha Mtaliano Carlo Ancelotti aliongoza Chelsea kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England na Kombe la FA ndani ya msimu mmoja. Na msimu huo, The Blues walipewa penalti 12.

Msimu wa 2013-14, Liverpool walipokaribia kabisa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu chini ya kocha Brendan Rodgers, kabla ya kushindwa dakika za mwisho, miamba hiyo ya Anfield, yenyewe pia ilipewa penalti 12 ndani ya msimu mmoja.

Arsenal ya kocha Arsene Wenger kwenye msimu wa 2006-07 yenyewe pia ilipewa penalti 12 kipindi hicho kikosi chao kilipokuwa na mastaa wengi matata, akiamo Thierry Henry, Robin van Persie na Cesc Fabregas kwa kuwataja kwa uchache.

Katika msimu ambao walibeba taji lao pekee la Ligi Kuu England, 1994-95, Blackburn Rovers nao walipewa penalti 12 ndani ya msimu huo, kama ilivuokuwa kwa Man United ya msimu wa 2018-19, iliyokuwa chini ya Jose Mourinho kisha kuja Ole Gunnar Solskjaer baada ya Mreno huyo kufukuzwa, yenyewe pia ilipewa penalti 12 ndani ya msimu mmoja.

Kwa ujumla wake, Man United kwenye michuano yote iliyocheza msimu huu, imepewa penalti 20 huku ikiwamo bado inaendelea kukipiga kwenye mikikimikiki ya Europa League, hivyo kuna uwezekano akaandika rekodi ya kupewa penalti nyingi zaidi msimu huu.

PENALTI NYINGI MSIMU MMOJA EPL

2019/20 – Man United, penalti 14

2015/16 – Leicester City, penalti 13

2004/05 – Crystal Palace, penalti 13

2009/10 – Chelsea, penalti 12

2013/14 – Liverpool, penalti 12

2006/07 – Arsenal, penalti 12

1994/95 – Blackburn, penalti 12

2018/19 – Man United, penalti 12

Advertisement