Man U yapigwa bao jingine Ulaya

Muktasari:

Na sasa La Gazzetta dello Sport linaripoti kwamba Paris Saint-Germain wameibuka mstari wa mbele kwenye vita ya kunasa huduma ya beki huyo, wakimwaandalia mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 10.2 milioni kwa mwaka.

NAPLE, ITALIA . MAISHA ndivyo yalivyo, mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama.

Si unajua kwamba Manchester United kwa muda mrefu wanatajwatajwa kwenye mpango wa kumsajili beki wa kati wa Napoli, Kalidou Koulibaly?

Basi sasa mpango huo unaweza kukwama kwa sababu kuna watu na pesa zao wameingilia kati na wanahitaji saini ya beki huyo wa kimataifa wa Senegal. Ni Paris Saint-Germain buana, ndio wanaomtaka beki huyo mwenye umri wa miaka 28.

Taarifa za huko Italia zinaweka wazi kwamba beki huyo kwa sasa yupo tayari kuachana na Serie A baada ya kukerwa na Napoli kumfuta kazo kocha Carlo Ancelotti.

Na sasa La Gazzetta dello Sport linaripoti kwamba Paris Saint-Germain wameibuka mstari wa mbele kwenye vita ya kunasa huduma ya beki huyo, wakimwaandalia mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 10.2 milioni kwa mwaka.

Kinachoelezwa ni kwamba mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo ameshaanza mazungumzo na wakala wa Koulibaly na kwamba wameshaweka mezani mkwanja wa Pauni 41 milioni na kwamba kwa mwaka unaweza kuongezeka kwa Pauni 4.2 milioni kutokana na kile timu itakachofanikiwa ndani ya uwanja.

Lakini, inaripotiwa Napoli wao wanataka Pauni 100 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo jambo linalozifanya timu nyingi kukwama kwenye kumsajili kutokana na mkwanja huo mrefu.