Man City yashinda rufaa, United yakomaliwa

Muktasari:

Taarifa zilizotoka leo Jumatatu Julai 13, 2020 England zimeeleza kuwa Manchester City imeshinda rufaa kwenye Mahakama ya Michezo (CAS) ya kuzuiliwa kutoshiriki michuano ya Uefa kwa misimu miwili baada ya kuvunja sheria ya usawa wa matumizi ya fedha.

MANCHESTER, ENGLAND. UKISIKIA bahati mbaya ndio hii, wakati Manchester United ipo bize kugombania nafasi ya tano ili ishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa msimu ujao, Manchester City imeshinda rufaa yake.

Taarifa zilizotoka leo Jumatatu Julai 13, 2020 England zimeeleza kuwa Manchester City imeshinda rufaa kwenye Mahakama ya Michezo (CAS) ya kuzuiliwa kutoshiriki michuano ya Uefa kwa misimu miwili baada ya kuvunja sheria ya usawa wa matumizi ya fedha.

Februari mwaka huu, Uefa iliitia hatiani klabu hiyo kwa kosa la kutumia pesa zaidi ya zile ambazo wanaingaiza, ambapo inadaiwa ubathilifu huo waliufanya kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, pia walishatakiwa kwa kutotoa ushirikiano kipindi cha uchunguzi.

Hukumu ya City ilikuwa ni kufungiwa miaka miwili kutoshiriki michuano ya Uefa pamoja na kutozwa faini ya Pauni 26.9 milioni. Lakini  walipinga hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa CAS.

Kupitia rufaa hiyo ambayo ilijadiliwa ndani ya siku tatu, leo Jumatatu saa 3:30 asubuhi majibu yake yalitoka ambapo City imefutiwa hukumu ya kutocheza misimu miwili ya Uefa, hivyo msimu ujao wanaruhusiwa kushiriki, pia faini yao ya Euro 30 milioni, imepunguzwa hadi Euro 10 milioni.

Taarifa ya Uefa ambayo ilithibitisha jambo hilo, ilikuwa inasema kuwa, CAS imefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na ushahidi uliotolewa na Uefa juu ya sakata hilo.

Baada ya City kushinda hukumu hiyo, hali imezidi kuwa mbaya zaidi kwa majirani zao United ambayo ilikuwa inaamini kuwa kwa kushika nafasi ya tano msimu ujao wangeshiriki ligi ya mabingwa kwa kuwa City asingeshiriki.

Mbali na kushinda rufaa hiyo City bado inatajwa kuwa na msala mwingine kwa chama cha soka nchin England (FA) ambacho pia kina sheria ya usawa wa matumizi kama ilivyokuwa kwa Uefa, fununu zinadai kwamba huenda wakahukumiwa na chama hicho.

Katika taarifa iliyotolewa na City wenyewe imeeleza namna wanavyowashukuru watu wote ambao walikuwa bega kwa bega na wao katika kuhakikisha inashinda rufaa yake.

City itakuwa na mchezo wa marudiano hatua ya 16 bora dhidi ya Real Madrid unaotarajia kupigwa Agosti, 7 mwaka huu, mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Febuary, City iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.