Man City wanahofia maisha yao Anfield

Muktasari:

Polisi wa Merseyside walikosolewa kwa jinsi walivyoshughulikia pambano la mwaka jana na namna basi la City lilivyoshambuliwa huku wakitaja njia ambayo basi la City litapita, lakini safari hii njia ya basi la City imefanywa kuwa siri.

MERSEYSIDE, LIVERPOOL . JOTO linapanda pale England. Kesho ni Liverpool dhidi ya Manchester City. Pambano linatazamiwa kuamua kwa kiasi fulani mbio za ubingwa wa England. Na sasa joto limepanda zaidi baada ya kugundulika kuwa wapinzani wanahofia maisha yao Anfield.

Maafisa wa Manchester City wameomba wahakikishiwe usalama wao Anfield pindi basi la timu yao litakapokuwa linawasili katika Uwanja wa Anfield kufuatia Liverpool kutoa tangazo la kutaka mashabiki wao waje na mabango mbalimbali kabla ya mechi.

City ina kumbukumbu ya kupokewa kwa chuki katika pambano la mtoano Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Liverpool mwaka jana na wenyeji wao walilazimika kuiomba radhi City kutokana na vurugu walizofanyiwa wakati wakiingia uwanjani.

Licha za vurugu za mwaka jana Liverpool walikuwa hawajaomba mashabiki wao kuja uwanjani na bendera na mabango lakini safari hii wametoa tangazo kwa mashabiki wao kuja uwanjani na kila walichonacho na tayari City wameelezea hofu yao kuhusu tangazo la Liverpool.

Polisi wa Merseyside walikosolewa kwa jinsi walivyoshughulikia pambano la mwaka jana na namna basi la City lilivyoshambuliwa huku wakitaja njia ambayo basi la City litapita, lakini safari hii njia ya basi la City imefanywa kuwa siri.

Ndani ya uwanja, Kocha wa City, Pep Guardiola amekuwa katika wakati mgumu kidogo baada ya kipa wake namba moja, Ederson kuumia katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Atalanta Jumatano usiku na nafasi yake ilichukuliwa na Claudio Bravo.

Bravo alipewa kadi nyekundu katika pambano hilo lakini kadi yake haitahusika katika pambano la kesho ambalo linatazamiwa kuwa kali na la kusisimua huku wachambuzi wengi wakishindwa kutabiri matokeo ya pambano hilo. Kiungo David Silva atakosekana katika pambano hili baada ya kuwa majeruhi huku akiungana na winga, Leroy Sane, beki Aymeric Laporte, kiugo Rodrigo na beki wa kushoto, Oleksandr Zinchenko ambao wote ni majeruhi. Kocha Guardiola alichezesha kikosi chake chote chenye nguvu kwa sasa katika pambano dhidi ya Atalanta lakini mshambuliaji Sergio Aguero, beki wa kati John Stones na beki wa pembeni, Kayle Walker ambaye aliingia kama kipa wakati Bravo alipopewa kadi nyekundu wanatazamiwa kuanza pambano la kesho Jumapili.

Kocha huyo Mhispaniola anaweza kulazimika kumrudisha kiungo wake Fernandinho kucheza kama beki wa kati huku akimuanzisha staa wake wa Ureno, Bernardo Silva katika upande wa kulia na kumuweka nje staa wa Algeria, Riyad Mahrez.

Kocha Jurgen Klopp anaweza kuingia majaribuni na kumpanga kiungo wake wa kimataifa wa England, Alex Oxlade-Chamberlain ambaye yupo katika fomu na amefunga mabao matatu katika mechi mbili zilizopita Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Genk. Staa huyo ameitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya England.

Kiungo Jordan Henderson ambaye hakuceza dhidi ya Genk anaweza kupisha njia kwa Oxlade-Chamberlain kuanza pambano hilo kama akishindwa kupona kwa wakati. Kiungo wa kimataifa wa Brazil, Fabinho ambaye yupo katika fomu aliwekwa nje katika pambano la Ligi Kuu lililopita kutokana na kuwa na kadi nne za njano na ni wazi ataanza katika pambano hili Anfeld. Beki staa wa kimataifa wa Croatia, Dejan Lovren kwa mara nyingine anatazamiwa kupangwa na nyota wa Uholanzi, Virgil van Dijk katika eneo la kati la ulinzi mbele ya Joe Gomez baada ya kuendelea kufanya vema tangu beki Joel Matip awe majeruhi.