Mambo mawili kuivusha Yanga kwa Township Rollers

Muktasari:

Katika mechi tano za mwisho ilizocheza hivi karibuni, ukiondoa ile dhidi ya Mlandege ambayo Yanga ilishinda mabao 4-1

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Yanga lina kazi mbili nzito za kufanya ndani ya siku nne ili iweze kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kusaka muunganiko wa kitimu na kuipa makali safu ya ushambuliaji ni majukumu mawili yanayopaswa kufanyiwa kazi na Yanga kabla ya mechi ya ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Ikihitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili isonge mbele, Yanga inakabiliwa na changamoto ya kikosi chake kukosa uelewano mzuri uwanjani ambayo isipofanyiwa kazi inaweza kuwagharimu katika mechi hiyo ya ugenini.

Katika mechi tano za mwisho ilizocheza hivi karibuni, ukiondoa ile dhidi ya Mlandege ambayo Yanga ilishinda mabao 4-1, wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakicheza zaidi kwa kutegemea uwezo binafsi wa mtu mmoja mmoja badala ya kucheza kitimu.

Hatua hiyo imechangia wapinzani wao kujipanga na kutibua mipango yao na kujikuta ikiwa katika wakati mgumu kupata matokeo mazuri kwenye mechi hizo.

Mfano katika mechi waliyocheza dhidi ya Rollers, Yanga ilikosa ubunifu hasa katikati mwa uwanja wa kutengeneza nafasi za mabao kutokana na viungo Mapinduzi Balama, Papy Tshishimbi na Mohammed Issa ‘Banka’ kutokuwa na muunganiko na uelewano mzuri.

Mbali na hilo, washambuliaji wa timu hiyo wamekuwa na changamoto ya kushindwa kujipanga sehemu sahihi, kukosa utulivu na umakini katika kutengeneza nafasi pamoja na kufunga mabao.

Washambuliaji wa Yanga, Juma Balinya na Sadney Urikhobi wamekuwa ama wakicheza mbali na lango, pia wamekuwa wakishindwa kuendana na kasi ya viungo na washambuliaji wa pembeni jambo linalowafanya ama wajikute hawapo sehemu sahihi pindi mpira unapopigwa kwenye lango la timu pinzani au kuwahi kabla na kuwapa mwanya mabeki kuwadhibiti.

Katika mechi nne za mwisho, Yanga imefunga mabao matatu tu yote yakifungwa na wachezaji wa nafasi ya kiungo Deus Kaseka, Papy Tshishimbi na Patrick Sibomana.

Ni bao moja kati ya hayo matatu ambalo lilifungwa kutokana na nafasi ambayo ilitengenezwa na Yanga ambalo lilifungwa na Kaseke kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Malindi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 huku mengine mawili, moja likiwa la mkwaju wa penalti na jingine likitokana na mpira wa kona.

Wakati Yanga ikikabiliwa na changamoto hiyo, Kocha Kenny Mwaisabula alisema kikosi cha Yanga kimekosa muunganiko wa timu kulinganisha na Simba au Azam.

“Bado hawaonyeshi kucheza kitimu, wanacheza mmoja mmoja, hii sio dalili nzuri kwa Yanga inaonyesha hata mechi yao ya marudiano na Township Rollers itakuwa na wakati mgumu kama wasipobadilika,” alisema Mwaisabula.

Kocha wa zamani wa Yanga, Fred Felix ‘Minzir’o alisema maandalizi ya Yanga hayajakidhi mashindano ya kimataifa.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema maandalizi ya Yanga imefanya ya hayajaonekana kufanya kazi.

“Alichosema Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera baada ya mechi na Leopards ni sahihi, unapofanya maandalizi, mazingira yaendane na yale ambayo utakwenda kucheza mechi, lakini katika mchezo na AFC Leopards ni tofauti,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.