Mambo haya kumrudisha Beno Kakolanya Yanga

Muktasari:

Utata wa ishu ya Beno umefikia hatua nyingine baada ya kipa huyo kuiandikia klabu yake hiyo barua ya kutaka kuvunja mkataba wake kishgeria.

MIEZI mitano imepita kipa wa Yanga Beno Kakolanya amekuwa nje ya kikosi hicho. Sababu kubwa ikiwa ni kocha wake, Mwinyi Zahera kukataa kumrudisha kikosini kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Zahera amezidi kushikilia panga hamtaki na anawashangaa wanaoendelea kujadili suala hilo, huku mashabiki wengine wakimsapoti kocha huyo na wengine wakipinga na kumtaka amsamehe.

Utata wa ishu ya Beno umefikia hatua nyingine baada ya kipa huyo kuiandikia klabu yake hiyo barua ya kutaka kuvunja mkataba wake kishgeria.

Hata hivyo, yapo mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kusababisha kurejea kwa kipa huyo, aliyekuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo kutokana na umahiri wake, kwenye kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria ambao kwa sasa kasi yao kwenye Ligi Kuu Bara ni moto na kuna kila dalili za kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Kifupi hili bado ni sakata na linaweza kufikia tamati kwa Kakolanya ama kuondoka mazima au hata akabaki kutokana na aina ya nyakati tunazoishi na yafuatayo ni mambo matano ambayo yanaweza kumrudisha Yanga kipa huyo.

Hatua za kuvunja mkataba

Kakolanya ameomba kuvunja mkataba. Hii ina maana ni yeye ndiye anatakiwa kuununua mkataba wake na tayari barua yake iko Yanga. Hata hivyo, ombi hilo Yanga wana haki ya kukataa au kulikubalia kwa kuwa bado ni mali yao halali, kwani bado anaendelea kuchukua mishahara na malipo ya ada ya usajili wake wa mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, endapo Yanga itahitaji kiasi kikubwa cha fedha katika kutaka fidia za kuvunjwa kwa mkataba huo, hili linaweza kuwa zito kwa upande wa Kakolanya.

Mfano Yanga inaweza kutaka hata Sh300 milioni au hata 1 bilioni, ndiyo, si wao wanasema walikuwa na matarajio gani kwa kipa huyo wakati wanamsajili.

Likitokea hili usishangae hatua inayofuata ni upande wa Kakolanya kuamua kurudi nyuma na kukaa meza moja na kutafuta suluhu ambayo inaweza kumrudisha klabuni hapo.

Matokeo Yanga vs Simba

Kama kuna kitu mashabiki hawapendi kwa timu zao hizi, ni kupoteza kwenye mechi hizi za watani. Kariakoo Derby ni habari nyingine na kila mtu hufuatilia kujua nini kitatokea. Habari ya kufungwa huwa inachukuliwa kwa uzito na kutafutwa chanzo.

Hapo sasa ndipo Yanga na mashabiki wake huzingatia kila idara kuanzia kipa hadi washambuliaji.

Katikati ya mwezi huu, Yanga inaweza kukutana na Simba. Hii ina maana, kama hali itakuwa hivi, langoni atasimama mmoja kati ya makipa Klause Kindoki, Ramadhan Kabwili au hata Ibrahim Hamid.

Ikitokea katika mchezo huo Yanga ikapoteza tena kwa makosa ya makipa wake moto wake utakuwa mzito na lolote ninaweza kutokea. Kuipata suluhu ya haraka ni kurudishwa kwa Kakolanya ambaye kiukweli kiwango chake ni zaidi ya makipa wote Yanga.

Lawama za Kindoki, Kabwili

Mashabiki wengi huwatazama makipa wa sasa Kabwili na Kindoki. Hawa ni wale wanaotaka Kakolanya arudishwe wakiwa hawana imani na makipa hao wengine.

Wakati mwingine kunaweza kutokea makosa yakawa ya mabeki, lakini lawama wakatupiwa wao.

Hawawaamini sana japokuwa wamekuwa wakiibeba timu yao tangu Kakolanya asimamishwe kucheza. Ni wakifanya makosa kwa kiasi kikubwa suala hilo litaleta msukumo wa kurudishwa kwa Beno.

Zahera kulegeza msimamo

Ukisikia Kakolanya karudi Yanga, basi ujue Kocha Zahera ndio kaamua, kwani ni yeye ndiye aliyemzuia kuidakia timu hiyo na kusimamia msimamo wake huo kwa miezi yote mitatu hadi sasa. Zahera hataki kumrudisha na alifika mbali zaidi akimlazimisha atimke Yanga kama anataka.

Ni nani pale Yanga anaweza kukubali Zahera aliyeikamata klabu kwa kuipa ubora mkubwa aondoke?

Hata hivyo, Zahera ni binadamu. Huwezi kujua labda atalegeza msimamo wake kama mwenyewe alivyowahi kusema. Anaweza akaamua kufungua nafsi yake na kulegeza msimamo wake huo na hii itakuwa ni fursa kwa Kakolanya kurudi Jangwani.

Kakolanya kuomba radhi

Kwa sasa Zahera ni kila kitu pale Yanga. Anapendwa na viongozi na mashabiki hauwaambii kitu kwa kocha wao huyo ambaye ameweza kuwafuta machozi kutokana na hali ya kiuchumi inayoendelea kwenye klabu hiyo.

Ukweli ni, Zahera ameshika panga lenye makali huku Kakolanya ameshikilia makali yenyewe. Akiamua kulivuta panga hilo basi kipa huyo linamkata.

Kakolanya hataki kujishusha lakini kama ataamua kufanya hivyo kwa kuomba radhi ili sakata hilo limalizike, ni wazi atajitengenezea nafasi nzuri ya kurudishwa golini kufanya mavitu yake.

Nyota Yanga kumwombe msamaha

Hii inaanza kwa Kakolanya mwenyewe, kisha wachezaji wa Yanga kupata msukumo wa kufanya hivyo ili kumsaidia mwenzao. Inaelezwa mpaka sasa wachezaji wa Yanga hawajaenda kumwombea kipa huyo kurudishwa kikosini na hii sio kawaida.

Zahera amewahi kuombwa mara kadhaa na wachezaji wake amsamehe mchezaji anayefanya makosa lakini kwa sasa mambo ni tofauti kutokana na msimamo wake kwa mchezaji huyo.

Hata hivyo, ikitokea Kakolanya akaomba radhi kisha wenzake nao wakamfuata Zahera na kushindilia msamaha huo, tusishangae kuona kipa huyo anarudishwa kundini na kuendelea kupambana na wenzake.