Malindi yaikazia Yanga usiku

Muktasari:

Bao la Yanga liliwekwa kambani na Deus Kaseke dakika ya 16 kabla ya kiungo mshambuliaji Mohammed Adam kuisawazishia Malindi SC zikiwa zimesalia sekunde chache kumalizika kwa mchezo huo.

WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Malindi usiku wa jana Alhamisi wameidindia Yanga na kutoka nao sare ya bao 1-1 wakiwasha taa ya kijani kwenye mechi yao dhidi ya Mogadishu City.
Mechi ilipougwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar ikiwa ni mechi ya kujipima nguvu kabla ya timu hizo hazijaanza majukumu ya kimataifa.
Bao la Yanga liliwekwa kambani na Deus Kaseke dakika ya 16 kabla ya kiungo mshambuliaji Mohammed Adam kuisawazishia Malindi SC zikiwa zimesalia sekunde chache kumalizika kwa mchezo huo.
Sare hiyo inawafanya Malindi kuingia uwanjani kesho dhidi ya Mogadishu City ya Somalia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho ikiwa kifua mbele kutokana na kujiweka vizuri kwenye michezo ya kirafiki. Wawakilishi wengine wa Zanzibar KMKM yenyewe itakuwa na kazi dhidi ya Despotivo de 1 Agosto kesho.
Yanga ni mchezo wake wa pili nakiwa visiwani humo baada ya juzi kuilaza 4-1 Mlandege SC na kesho itakuwa uwanjani kucheza na Township Rollers kwenye Uwanja wa Taifa katika kipute cha Ligi ya Mabingwa Afrika.