Makonda amjibu Kikwete

Muktasari:

Yanga ilikuwa haina uwanja wa mazoezi wa kwao, huku watani wao Simba nao hawana uwanja wa mazoezi ingawa wameanza kuutengeneza uwanja huo ambao awali uliahidiwa kukamilika Februari mwaka huu na baadaye ujeni kusimama kwani nyasi zao zilizuiliwa na ziliporuhusiwa ujenzi haukuendelea kutoka na mvua.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni kama amemjibu Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kutoa zawadi ya uwanja kwa klabu ya Yanga.
Awali, Dk  Kikwete alisema akiwa madarakani aliichangia Simba Sh 30 milioni walipokuwa wananunua uwanja wao uliopo Bunju wakati huo wakiwa chini ya Mwenyekiti wao Aden Rage.
Akizungumza wakati wa hafla ya Kubwa Kuliko iliyoandaliwa na Yanga iliyofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee, Makonda alisema baada ya watu wengine kuchangia pesa yeye ameona atoe zawadi ya tofauti.
"Baada ya Rais mstaafu kutoa uwanja kwa Simba basi na mimi natoa uwanja kwa Yanga kule Kigamboni, uwanja huu utakuwa wa klabu ya Yanga," anasema Makonda.
Aliongeza kuwa, Jumatatu atakuwa na wataalam wa ardhi katika ofisi yake na hapo itatengenezwa hati yenye jina la klabu hiyo.
"Nilikuwa nimekaa na Kaya (Omary, Kaimu Katibu wa Yanga), nikawa namuuliza uwanja unachukua kama heka ngapi na aliponambia ndio maana nimetoa uwanja," alisema.
Yanga ilikuwa haina uwanja wa mazoezi wa kwao, huku watani wao Simba nao hawana uwanja wa mazoezi ingawa wameanza kuutengeneza uwanja huo ambao awali uliahidiwa kukamilika Februari mwaka huu na baadaye ujeni kusimama kwani nyasi zao zilizuiliwa na ziliporuhusiwa ujenzi haukuendelea kutoka na mvua.

Hata hivyo, Yanga ina eneo la Kaunda ambalo halitumiki na limekuwa likijaa maji ambapo mara kadhaa viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakipambana kuujenga ikiwemo kujaza kifusi.
Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alimshukuru Makonda lakini aliwekwa wazi kwamba uwanja wa Kaunda utabaki kuwa mali yao na huko Kigamboni watajenga kitega uchumi kingine.