Makocha watoa mtazamo ligi ya wanawake

Muktasari:

Huu utakuwa msimu wa utakuwa msimu wa nne kucheza Ligi kuu ya Wanawake Tanzania Bara, tangu ianzishwe mwaka 2017 chini ya aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi.

LIGI  Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, inatazamwa kuwa na ushindani mkali msimu huu, kama walivyozungumza makocha baadhi yao kwamba timu zimesajili vizuri na chipukizi wanakuja juu.
Kocha wa JKT Queens, Ali Ali amesema ushindani wa ligi msimu huu utatokana na usajili uliofanywa na timu ambao aliufafanua unatokana na ligi hiyo kuanza kupendwa na jamii.
Amesema wakati ligi inaanza haikuwa na mvuto mkubwa kama ulivyo sasa ambapo timu zinajipanga kuonyesha ushindani wa kweli na wachezaji wanaona ni ajira.
"Tofauti na ligi ilivyoanza mwaka 2017 haikuwa nguvu kubwa kama ilivyo sasa ambapo Simba na Yanga zimeingia humo ambazo zina mashabiki lukuki,'
"Mpira wa wanawake sasa umegeuka ni ajira mvuto kwa mashabiki kama ilivyo kwa wanaume, ndio maana timu zinajiandaa kikamilifu, mchezo wetu na Baobab Queens ambao tunaanzia ugenini, hautakuwa rahisi,"amesema.
 Kwa upande wa kocha wa Alliance, Eziekel Chobanka ameuzungumzia mchezo wao na Kigoma Sisterz utakaopigwa Oktoba 26, Uwanja wa Nyamagana kwamba utakuwa na ushindani mkali.
"Timu zimesajili, soka la wanawake linakuwa siku hadi siku hata kama halina udhamini kama ilivyo kwa wanaume ila vipaji ni vikubwa, msimu ni mgumu, zikichezwa mechi tatu tutaona nani kajipanga zaidi,"amesema.
Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi amesema wanafungua ligi na Ruvuma Queens iliopanda daraja msimu huu, hivyo watahitaji kuonyesha uzoefu kwa kupata matokeo.
"Tunahitaji kuwa mfano kwa kuonyesha uzoefu kwa timu ambazo zimepanda ligi kwa msimu huu, ingawa hatuwezi kuzidharau kwa sababu zimesajili na tunatarajia ziibue ushindani wa juu,"amesema.