Makocha wang’aka Amunike kutimuliwa

Muktasari:

Hata hivyo, uamuzi wa TFF kuachana na Amunike umeibua mjadala kwa baadhi ya makocha wa soka nchini ambao walisema uamuzi huo umefanyika kutokana na presha ya mashabiki kwa kuwa hauna uhalisia katika utendaji kazi wa nyota huyo wa zamani wa Barcelona.

Dar es Salaam. Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likitangaza kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na Kocha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike, baadhi ya makocha nchini wametoa maoni tofauti.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, makocha waliozungumza na gazeti hili, walisema uamuzi wa TFF wa kuachana na Amunike umetokana na mihemko.

Jana TFF kupitia Ofisa Habari, Clifford Ndimbo ilisema wamekubaliana na Amunike kusitisha mkataba ikiwa ni siku chache tangu Taifa Stars irejee nchini ikitokea Misri ilipokuwa ikishiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Ndimbo alisema TFF inatarajiwa kutangaza kocha wa muda atakayeinoa Taifa Stars katika mechi za fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan).

Taifa Stars inatarajia kuanza dhidi ya Kenya katika mchezo unaotarajiwa kupigwa Dar es Salaam, Julai 27 kabla ya kwenda ugenini kucheza mechi ya marudiano.

“Makocha wa muda watatangazwa baada ya kamati ya dharura ya kamati ya utendaji kukutana Julai 11,” alisema Ndimbo.

Hata hivyo, uamuzi wa TFF kuachana na Amunike umeibua mjadala kwa baadhi ya makocha wa soka nchini ambao walisema uamuzi huo umefanyika kutokana na presha ya mashabiki kwa kuwa hauna uhalisia katika utendaji kazi wa nyota huyo wa zamani wa Barcelona.

Makocha wafunguka

Wakati TFF ikisema inasaka mrithi wa muda wa Amunike, Kocha wa Polisi Tanzania, Sulemani Matola alisema uamuzi wa kuachana na Amunike umetokana na presha ya mashabiki na si vinginevyo.

“Wadau wa mpira wanataka vitu vikubwa ambavyo kiuhalisia vinahitaji muda ili Tanzania ifike huko tunakofikiria katika soka,” alisema Matola.

Alisema awali Tanzania ilionyesha ilikuwa na malengo ya kufuzu kucheza fainali hizo, lakini si kushinda, jambo ambalo Amunike alifanikisha.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema kuondoka kwa Amunike kuna kitu nyuma ya pazia huku akisisitiza kwamba, tatizo la Watanzania wanapenda kuingilia kazi za kitaalamu za watu wengine.

“Kilichomuondoa Amunike hakuna shaka ni matokeo ambayo Stars imepata Afcon, lakini kama TFF ilikubaliana na kocha akachukue ubingwa, basi iko sahihi kuachana naye kwa kuwa hajatimiza malengo,” alisema Mwaisabula huku akihoji.

“Kama Amunike angekuwa Kocha wa Senegal halafu Kocha wa Senegal ndiye angekuwa wa Stars, Tanzania tungefuzu hatua ya 16-Bora? Kumshambulia Amunike kwa matokeo ya Afcon ni kumuonea kwani tatizo sio kocha ni mfumo wetu wa soka, kila mdau wa soka ni kocha, kitu ambacho haiwezekani,” alisisitiza. Alisema Senegal na Algeria ambazo zilizokuwa kundi moja na Taifa Stars zimewekeza ndiyo sababu zimefuzu hatua ya robo fainali.

“Hata huyo kocha mwingine watakayemtambulisha yatamkuta hayo hayo tu, tunashindwa kutibu tatizo, tunawalaumu makocha, aliletwa Mayanga, Mkwasa, Poulsen na wengine wote tumewaona hawafai,” alisema Mwaisabula.

Naye kocha nguli anayeinoa moja ya klabu ya Ligi Kuu ambaye aliomba hifadhi ya jina alisema, kuachana na kocha wakati wachezaji hawakucheza kwa kiwango bora si jambo la busara.

“Tangu tumeanza kubadili makocha, Stars imebadilika nini? Alihoji kocha huyo ambaye alisema kwenye Afcon Tanzania ilikwenda kuangalia timu nyingine zikicheza mpira, lakini si kushindana.

“Niliwahi kusema kabla, tunakwenda Misri kuwaangalia wenye mpira wao wakicheza mpira, lakini Watanzania wengi waliwaza mambo makubwa, kuna tofauti kati ya Afcon na Chalenji au Super Ligi, lakini hatutaki kukubaliana na ukweli huo,” alisema.

Alisema katika Afcon, wachezaji wa Tanzania ambao waliendana na mashindano ni Mbwana Samatta na Simon Msuva, waliosalia hawakuwa na kiwango hicho.

“Tulianza kuingiza siasa kwenye mpira, wengine walidiriki hadi kuhoji mbona kocha kamuacha fulani, tukasahau siasa za mpira haziwezi kutupa matokeo, tatizo liko kwenye mfumo, huwezi kukatisha duara kama yai ili kuwahi mafanikio, hata akija kocha mwingine, tusipoweka mfumo mzuri bado ataonekana hafai,” alisema.

Wanasiasa

Awali, baadhi ya wabunge walimshambulia Amunike baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 2-0 na Senegal katika mchezo wa kwanza wa Kundi C.

Spika wa Bunge Job Ndugai na baadhi ya wabunge walikwenda Misri kutoa hamasa wakati Taifa Stars ikijiandaa kuivaa Senegal, baadaye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam naye alikwenda kutoa hamasa timu hiyo ilipokuwa ikijindaa kuivaa Kenya.

Rekodi

Tangu alipojiunga na Taifa Stars kwa mkataba wa miaka miwili Agosti mwaka jana, Amunike ameiongoza timu hiyo kushinda mechi mbili, ametoka sare mara mbili na kufungwa michezo sita.

Mechi hizo ni zile za kufuzu Afcon ambapo aliiongoza Taifa Stars kupata suluhu na Uganda, alifungwa 3-0 na Cape Verde, 1-0 dhidi ya Lesotho na alishinda 2-0 katika mechi yake na Cape Verde kabla ya kuilaza Uganda 3-0.

Pia ameiongoza Taifa Stars katika michezo miwili ya kirafiki na kutoka sare ya bao 1-1 na Zimbwabwe kabla ya kufungwa 1-0.

Katika fainali za Afcon, timu hiyo ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Senegal, ilichapwa 3-2 na Kenya kabla ya kulala 3-0 ilipovaana na Algeria. Mara ya kwanza Taifa Stars kucheza Afcon ilikuwa mwaka 1980 nchini Nigeria.