Makocha hawa wamekalia kuti kavu

JUZI Ijumaa Ligi Kuu Bara iliingia raundi ya tano kwa kushuhudia Wazee wa Kupapasa, Ruvu Shooting ikipasuka ugenini mjini Dodoma kwa mabao 2-0 mbele ya wenyeji wao Dodoma Jiji.

Kivumbi cha ligi hiyo kimeendelea jana na kesho kitamaliza raundi hiyo ya tano kwa timu 16 kusaka alama tatu na kujiwekea mazingira mazuri ya kubeba ndoo ya msimu huu.

Watetezi, Simba wanaifukuzia Azam FC inayoongoza msimamo (hii ikiwa ni kabla ya mechi za jana), huku Mbeya City ikiwa na hali mbaya ikiziburuza klabu nyingine 17 zinazoshiriki ligi hiyo.

Mbeya City kabla ya mechi ya jana dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa haijafunga bao lolote wala kuwa na pointi licha ya kucheza mechi nne za ligi hiyo, huku wageni wa ligi, Gwambina FC ambayo jana ilikuwa nyumbani jijini Mwanza kuikaribisha Ihefu, ilikuwa nayo haina bao, licha ya kumiliki alama moja (kabla ya jana).

Achana na Mbeya City na Gwambina na matokeo yao kabla ya mechi za jana, ukweli ni kwamba kuna makocha wana nafasi ndogo ya kumaliza msimu kama hawatajipanga sawa, hata kama ni mapema mno kuanza kuwahukumu wakufunzi hao kwa mechi walizocheza mpaka sasa.

Mwanaspoti linakuletea majina ya makocha ambao wanaweza kusepeshwa muda wowote kama hawatarekebisha mambo ndani ya vikosi vyao wakati ligi ikienda mapumziko ya wiki moja kupisha mechi za kimataifa zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Mbali na makocha hao tayari Yanga ishamtimua kocha wake Zlatko Krmpotic licha ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union. Krmpotic amekuwa kocha wa kwanza kwa msimu huu kuondolewa.

Hitimana Thierry - Namungo FC

Alitua kwenye kikosi hicho wakati Namungo FC ikiwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) akitokea Biashara United na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu.

Uongozi ulimwamini na kuendelea kuwa naye kwa msimu wa kwanza wa Ligi Kuu na kuiwezesha kumaliza nafasi ya nne huku ikitinga fainali ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) na kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, Hitimana hadi sasa hana mkataba na timu hiyo na uongozi umekiri hilo, lakini matokeo mabovu ya mwanzo wa ligi yanaweza kumfanya kocha huyo kuachana nao.

Hitimana mara zote anaeleza hataki kulaumiwa kwa kile kinachoendelea kwenye kikosi chake hasa matokeo hayo maana asilimia kubwa ya usajili sio pendekezo lake, na bila shaka hatakubali kuchafua ‘CV’ yake.

Fulgence Novatus - Gwambina FC

Baada ya kutimuliwa Namungo FC misimu miwili iliyopita zali la mentali lilimwangukia kwa vijana hao kutoka Misungwi, Mwanza ikiwa ndio kwanza inatupa karata yake kwenye FDL.

Novatus alitesa vibaya sana huko FDL huku wapinzani wakiomba poo! Si unakumbuka hata kwenye ule mchezo wa ASFC dhidi ya Yanga pale Uwanja wa Uhuru? Gwambina iliupiga mwingi sana, sema bahati haikuwa yao ilipokubali kulala kwa bao 1-0.

Ilikuwa kama vile Simba aliyejeruhiwa, akarejea FDL na kasi yake na kufanikiwa kuvuna alama tatu na kuwa timu ya kwanza kupanda Ligi Kuu na ilimaliza msimu na alama 47 huku ikipoteza michezo mitatu kati ya 22.

Mabosi wakamwamini na kumpa timu aendelee nayo hadi Ligi Kuu. Licha ya ujio wa Mwinyi Zahera lakini haikuzuia kuwa kwenye kiti chake. Kasi waliyoanza nayo kwenye ligi inaleta shaka kama atabaki hadi mwisho, kwani imepoteza michezo miwili na kupata suluhu moja dhidi ya Kagera Sugar.

Khalid Adam - Mwadui FC

Msimu wa juzi ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya 17 kwa kuvuna alama 44 sawa na Kagera Sugar pamoja na Stand United ‘Chama la Wana’ ambayo inateseka huko kwenye FDL.

Mwadui iliponea chupuchupu baada ya kushinda 2-1 mchezo wake wa mwisho kwenye hatua ya mtoano dhidi ya Geita Gold na msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 11 ikiwa na alama 47.

Katika mechi iliyocheza imepoteza michezo yote mitatu, huku ikiafunga bao moja kwenye mchezo ambao walilala 2-1 dhidi ya KMC.

Hapa kuna mambo mawili ya kuangalia - kama sio Adam kuondoka ili kulinda heshima yake, basi uongozi unaweza ukafanya uamuzi mgumu ili kulinda chama lao.

Amri Said - Mbeya City

Ukipenda muite Jaap Stam, beki kisiki wa zamani kwenye kikosi cha Msimbazi. Wanaomjua vizuri au wale wakongwe wenzangu, basi tupeane tano kidogo.

Mbeya City tangu ilipoachana na Juma Mwambusi, Novemba 30, mwaka jana, imekuwa ikiendelea kupita kwenye mapito magumu na kuifanya kuwa moja ya timu isiyotabirika.

Kama sio Stam kuachana nao basi uongozi unaweza kuvunja ndoa hiyo endapo wataendelea kupata matokeo ya hovyo maana msimu uliopita ilipita kwenye tundu la sindano baada ya kujikomboa kupitia hatua ya mtoano mbele ya Geita Gold kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo wa kwanza kutokaa sare ya bao 1-1 ugenini na nyumbani kushinda bao 1-0.