Makocha hawa hawana maisha klabuni

Muktasari:

Siyo Yanga pekee inayoonekana ndoa yao na Kocha Mwinyi Zahera kuelekea ukingoni, bali kuna timu kadhaa maisha yao na makocha wao yako shakani iwapo mambo yataendelea katika staili ya sasa.

LIGI Kuu inashika kasi kwelikweli. Kwa upande wa bingwa mtetezi, Simba SC mambo ni safi kwa kocha Patrick Aussems kutokana na matokeo mazuri wanayovuna vijana wake kwenye ligi hiyo na kuzidi kuchanja mbuga kileleni wakiwa na pointi 18.

Wakati mambo yakiwanyookea wakali hao wa mtaa wa Msimbazi, hali imekuwa tofauti kwa mpinzani wao wa jadi, Yanga ambao juzi Jumapili wamechezea kichapo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids kutoka Misri, uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Kwa sasa wanasubiri kwenda kumalizana nao wiki ijayo nchini humo.

Siyo Yanga pekee inayoonekana ndoa yao na Kocha Mwinyi Zahera kuelekea ukingoni, bali kuna timu kadhaa maisha yao na makocha wao yako shakani iwapo mambo yataendelea katika staili ya sasa.

MWINYI ZAHERA - YANGA

Kocha huyo alitua nchini mwaka jana akichukua mikoba ya George Lwandamina akisaini mkataba wa miezi sita na baadaye uongozi ukaridhishwa na mwenendo wa timu iliyokuwa ikipita kwenye ukata, lakini ikivuna matokeo mazuri kabla ya kuanza kupoteana katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita.

Matokeo ya awali katika msimu huo yaliwafanya mabosi wa Yanga kumpa Zahera mkataba wa miaka miwili kutokana na kazi safi aliyoifanya, lakini msimu huu mambo yamekuwa tofauti, kwani amechokwa na mashabiki wanaohitaji aondoke.

Juzi baada ya Yanga kupoteza mchezo dhidi ya Pyramids, mashabiki hawakuwa wavumilivu kwani walisikika majukwaani wakiimba aondoke na kuonyesha mabango wakimtaka kocha huyo aachane na timu yao.

Yanga ilianza Ligi Kuu msimu huu vibaya kwa kufunga bao 1-0 na Ruvu Shooting kisha ikalazimishwa sare ya mabao 3-3 na Polisi Tanzania kabla ya kuja kuvuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union lililofungwa na Abdulaziz Makame, na baadaye kuifunga Mbao FC bao 1-0.

Kwenye michuano ya kimataifa, Yanga ilianza safari hiyo kwa kutoshana nguvu ya bao 1-1 na Township Rollers katika Uwanja wa Taifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika - mabao ambayo yalifungwa na Phenyo Serameng dakika ya nane upande wa Rollers wakati lile la Yanga likifungwa na Patrick Sibomana dakika ya 86 kwa penalti.

Katika mchezo wa marudiano Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini lililofungwa na Patrick Sibomana dakika ya 40. Kisha, baada ya hapo, timu hiyo ilisonga mbele na kukutana na Zesco ya Zambia na kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa, Septemba 14, Yanga ilibanwa mbavu kwa kufungana bao 1-1 yaliyofungwa na Sibomana dakika ya 25 kwa penalti kabla ya Thaban Kamusoko kusawazisha katika dakika ya 90 kwa upande wa Zesco.

Hata hivyo, Yanga ilikubali kulala kwa mabao 2-1 katika mchezo wa pili uliopigwa wiki mbili baadaye, akianza Jesse Jackson Were kufumania nyavu za Yanga dakika ya 25, kisha Sadney Urikhob kusawazisha dakika ya 31, lakini bao la

kujifunga la Abdulaziz Makame katika dakika ya 79 liliwapa ushindi Zesco na Yanga kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

JUMA MWAMBUSI - MBEYA CITY

Katika michezo sita ya Ligi Kuu, timu ya Mbeya City haijashida hata mmoja ikiwa inakamata nafasi ya 19, ikivuna alama nne kutokana na sare ilizoambulia.

Mbeya City ilianza Ligi Kuu chini ya Kocha Ramadhan Nswanzurwimo, lakini baadaye akatimkia Singida United inayoburuza mkia baada ya kuachana na Fredy Felix Minziro ambaye kwa sasa ametimkia Pamba FC ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mwambusi ndiye aliipandisha Mbeya City Ligi Kuu msimu wa mwaka 2013/14, lakini mwendelezo wa matokeo mabovu ya ligi msimu huu ni ishara mbaya kwake kuendelea na maisha ndani ya timu hiyo, huku mchezo uliopita akikubali kulala nyumbani kwa kichapo cha mabao 4-1 ya Kagera Sugar.

JACKSON MAYANJA - KMC

Siyo kocha mgeni kwenye soka la Bongo, alishaifundisha Kagera Sugar na baadaye Simba SC, lakini sasa katua Tanzania akikinoa kikosi cha KMC ambacho kiliachana na Etienne Ndayiragije aliyekwenda Azam FC kabla ya kutua zake Taifa Stars.

Wakati Ndayiragije akiisaidia KMC kumaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita na kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika, Mayanja hakuweza kufanya vizuri katika michezo hiyo - ilianza kwa suluhu dhidi ya Kigali FC kabla ya kulala kwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa na kutupwa nje.

Kwenye Ligi Kuu mpaka sasa imecheza michezo mitano ikishinda mmoja dhidi ya Namungo FC ilipoifunga bao 1-0 katika Uwanja wa Chamazi Complex, kisha sare ya bao 1-1 na Ndanda FC na kulazimishwa suluhu na JKT Tanzania, huku ikifungwa 1-0 na Azam FC na baadaye kulala 2-0 mbele ya Wagosi wa Kaya - Coastal Union.

MALALE HAMSINI - NDANDA FC

Kocha Malale Hamsini, maisha yake ndani ya Ndanda FC yako hatarini huku Mwanaspoti likidokezwa kwamba amepewa michezo mitatu ili kuona maendeleo ambayo yataamua kama ataendelea na timu au atatimuliwa.

Kocha huyo alitua kwenye kikosi hicho akichukua nafasi ya kocha Khalid Adam ambaye kwa sasa yupo Mwadui FC. Mpaka sasa Malale amekiongoza kikosi hicho kwenye michezo saba, lakini hajashinda hata mmoja huku ikiambulia sare nne. kufungwa michezo mitatu ikiwa katika nafasi ya 18.

Wamzungumzia Zahera

Mwanasoka wa zamani wa Yanga, Ali Mayay anasema, “bado mapema kwa uongozi na mashabiki wa Yanga kumhukumu Zahera na kumuondoa kutokana na matokeo anayoyapata, anapaswa kupewa muda zaidi wa kujipanga kwa sababu kufungwa na Pyramids si kigezo cha kuanza kumuona kuwa amefeli kukiendesha kikosi hicho wakati msimu uliopita alifanya mazuri licha ya kuwa na kikosi kibovu.”

Anasema presha ambayo anaipata kocha yeyote kutoka kwa mashabiki siku zote inakuwa hivyo - kwa kuwa mashabiki wanapenda matokeo mazuri, ndio maana wanalazimisha vitu ambavyo uongozi unapaswa kuwa makini kuvifanya kwewenye uamuzi.

Kocha Kennedy Mwaisabula anasema Yanga ilizidiwa kila idara na Pyramids na kwa muda mrefu kikosi hicho kinaonekana bado hakijakaa sawa, hivyo Zahera hapaswi kuangaliwa kama chanzo cha kutofanikiwa, bali kiufundi kuna vitu vingi ikiwemo kuwapa muda wachezaji waliosajiliwa msimu huu.