Majeraha yabomoa ukuta wa liverpool

Klabu ya Livepool ya England imepata pigo katika safu ya ulinzi baada ya beki wake wa kati, Virgil Van Dijk kupata majeraha ya goti ambayo yanaweza kumuweka nje kwa muda mrefu.

Alipata majeraha hayo siku ya Jumapili katika mechi yao ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Everton katika Uwanja wa Goodison Park baada ya kugongana na kipa wa Everton Jordan Pickford.

Kuumia kwa beki huyo ambaye msimu wa mwaka jana alikuwa mchezaji bora wa UEFA na wa EPL kumebomoa ukuta wa klabu hiyo ya London ambao mara zote umekuwa imara kutokana na ubora wake.

Ilikuwa dakika ya 10 wakati beki huyo akiwa amepanda kwenda kushambulia akiwa katika kasi ndani ya 18 aliingia kuwahi mpira ili afunge ndipo kipa wa Everton alitoka kwa kasi na kujikuta akigongana naye.

Shinikizo kubwa la uzito wa kipa huyo lilipiga katika eneo la goti la kulia la beki huyo toka Uholanzi na kulazimisha kwenda uelekeo hasi ambao ulisababisha kujeruhiwa kwa nyuzi ngumu ya goti.

Nyuzi hii ijulikanayo kitabibu kama Anterior Cruciate Ligament (ACL) ambayo huwapo katikati ya goti inayounganisha mfupa mkubwa wa paja na wa chini ya goti.

Kocha wa Liverpool siku ya Jumatatu aliwaeleza wanahabari kuwa wamepata pigo kwa safu ya ulinzi na watafanya kila linalowezekana kumuwezesha Van Dijk uponaji mzuri wa haraka na uhakika.

Alisema kuwa kwa namna klabu inavyosubiri kupona kwake ni kama vile mke mwema anayemsubiri mume aliye kifungoni.

Vilevile kocha huyo aligusia pia kuhusu kuwa nje kwa kiungo wake mpya mkabaji Thiago Alicantara na beki wa kati Joel Matip ambao nao ni majeruhi.

Wachezaji hawa nao ni muhimu kwa klabu hiyo, lakini kwa sasa wana majeraha ambayo yanaweza kuwaweka benchi.

Jumanne usiku Ligi ya Mabingwa Ulaya iliendelea kwa ngazi ya makundi ambapo Liverpool ilicheza na Ajax.

Kukosekana kwa beki huyo na mwenzake Matip, pamoja na kiungo mkabaji Thiago kunaweka pigo katika ukuta wa Liverpool kwenye eneo la ulinzi.

Kama ilivyo kwa wachezaji waliowahi kupata aina hii ya jeraha ni dhahiri kuwa naye atakosekana kwa muda mrefu kutokana na eneo hilo kuhitaji muda mrefu ili kupona na kuwa imara kama awali.

MAJERAHA YA LINGAMENTI

Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa mchezaji huyo amepata jeraha la goti la kulia kwa kuchanika nyuzi ngumu ya ligamenti iliyopo mbele ya goti katikati.

Kitabibu nyuzi hii inajulikana kama Anterior Cruciate Ligament kifupi ni ACL - ndiyo mhimili mkuu wa ungio la goti ikiwa eneo la katikati ikiunganisha mfupa mkubwa wa paja na wa chini ya goti.

Jeraha alilopata la ligamenti linaainishwa kama daraja la tatu ambayo nyuzi hiyo hukatika pande mbili na kuachana au kukwanyuka katika mfupa uliojipachika.

Kwa kawaida majeraha ya ligamenti huainishwa katika aina tatu za majeraha. Aina ya kwanza huwa ni kujivuta kupita kiwango na ya pili ni kuchanika pasipo kuachana pande mbili.

Daraja la tatu huwa ni jeraha baya linalohitaji upasuaji kama sehemu ya matibabu jambo linalochagia mchezaji kukaa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza jeraha la upasuaji.

Tayari Klabu hiyo imeishaeleza kuwa beki huyu anaendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi kuthibitisha ukubwa wa jeraha na huenda akafanyiwa upasuaji wa kisasa wa matundu.

Kwa namna tukio lilivyoonekana huenda ni Jeraha ni kubwa kwani alionekanekana akikunja sura kutokana na ukali wa maumivu huku akilishikilia goti hilo la kulia.

Aina hii ya majeraha huweza kuchukua muda mrefu kupona na kurudi tena uwanjani, jeraha hili linaweza kumweka nje kwa zaidi ya miezi 9 mpaka mwaka.

Aina hii ya jeraha ndilo pia lilimpata mchezaji mwezake Alex Oxlade-Chamberlain na kumweka nje msimu mzima wa 2018/19 na badaye alipona na kuendelea kucheza kama hapo awali.

Kwa aina ya upasuaji atakaofanyiwa huwa una matokeo mazuri na faida yake kubwa ni kuwa jeraha la upasuaji huwa ni dogo ukilinganisha na upasuaji wa kizamani.

Mpaka dakika hii haijaweka wazi ni hospitali gani au daktari gani ambaye anatarajia kumfanyia beki huyu aliyeupa mafanikio makubwa tangu atue klabuni hapo.

Tayari FA imeishachunguza tukio zima la kuumia kwake na imeona kuwa lilikuwa ni tukio la kimchezo, haikua rafu ya makusudi hivyo kipa wa Everton hakuchukuliwa hatua zozote.

Kipa huyo alikuwa muungwana zaidi kwa kumwomba msamaha beki huyo na kumweleza hakukusudia kufanya hivyo, alimpa pole beki huyo na kumtakia heri ya kupona haraka.

Kitabibu aina hii ya majeraha yanaweza kutofautiana kati ya mchezaji na mchezaji katika uponaji, tusubiri kwa Van Dijk tuone namna atakavyofanyiwa upasuaji na kupona.