Maisha ya Morrison, Yanga yameenda kasi sana

Muktasari:

Yanga walimsajili Morrison kwenye dirisha dogo la msimu huu kwa mkataba wa miezi 6 unaoisha Julai. Amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu

MAISHA yanaenda kwa kasi sana. Juzi Bernard Morrison alikuwa shujaa Jangwani, ghafla leo amekuwa kituko. Ndio, Morrison aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo miezi sita tu iliyopita aliwafanya Yanga waliimbe jina lake.

Waliokuwa wakilitambia mitaani baada ya mechi ya Machi 8, leo hawataki kulisikia. Ile friikiki yake matata ya dakika ya 44 iliyotaka kumvunja mbavu Aishi Manula, ilimpaisha winga huyo Mghana.

Bao lile lilimpa heshima kubwa na pia liliwapa heshima zaidi mashabiki wa Yanga ambao hawakuamini kama Mnyama angekufa Taifa siku ile. Kila shabiki wa Yanga, hakuwa na amani uwanjani wakati muda ukizidi kuyoyoma.

Sura zao zilionyesha hivyo. Kasi ya nyota wa Simba iliwatisha. Iliwakumbusha mechi yao ya kwanza iliyopigwa Januari 4. Simba ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0. Dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza, waliongeza la pili kupitia Deo Kanda. Walijua wanazikoga nyingi.

Hata hivyo, shuti la mwana ukome la Mapinduzi Balama na jingine la Mohammed Issa ‘Mo Banka’ aliyejichanganya mbele ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ yakawafutia aibu. Kasi ya Simba iliwanyima raha na wakajua muda wote mambo yangetibuka. Baadhi huenda walikuwa wakiomba angalau mapumziko yafike ngoma ikiwa bilabila.

 Hata hivyo faulo ya Jonas Mkude dhidi ya Morrison, iliwapa faraja. Faulo ilitokea nje kidogo ya 18 na mshale wa dakika ukisoma zimesalia sekunde chache kabla ya mapumziko. Morrison aliamua kuipiga mwenyewe na kumtesa Manula. Bao hilo liliwatia wazimu Wanayanga.

Furaha ilizidi baada ya dakika 90 kumalizika, mnyama akiwa amechinjwa Taifa kama utani. Sasa kila shabiki akawa analitambia jina la winga huyo mtata. Wengine wakafikia hatua ya kuyaandika magari yao jina la Mghana huyo. Kama sio kuandika Morrison basi ilikuwa ni BM33. Jina hilo likawa linawanyima raha mashabiki wa Simba. Kila walipokuwa wakitajiwa wanatetemeka na kunywea mbele ya wenzao wa Yanga. Simba walipata ganzi na walikatwa stimu kweli.

Hata inaelezwa mabosi wa Msimbazi wakaona isiwe tabu. Wakapenyeza walichopenyeza kwa msela sana, naye akaliamsha dude. Ingawa mabosi wa Simba wamekuwa wakikanusha uvumi huu, lakini inadaiwa Morrison aliwekewa mzigo wa maana mezani ukamchanganya.

Akalianzisha kwa kugomea safari ya kwanza ya Kanda ya Ziwa. Kisha akaja kulitifua kambini kiasi cha kumchefua Kocha Luc Eymael. Yanga wakasema walishamuongezea mkataba mpya wa miaka miwili, japo fedha walikubaliana kuwekewa baadaye.

Ila ule mzigo wa mtaa wa pili ulikuwa mzito kuliko wa vigogo wa Jangwani. Naye ametumwa fedha na watu wake. Kawaruka. Kisha wakafikishana ofisi za TFF. Yeye akiupinga mkataba, Yanga wakisisitiza jamaa anazingua. Mashabiki wakabaini kumbe BM33 ni msaliti. Wakambadilikia. Baadhi hawamtaki hata kumsikia kwa madai ni wao waliomkuza kwa lile bao dhidi ya mnyama. Ni kama anayefuga nyoka.

Anamlisha mwenyewe unga na nyama. Joka likuwa na kisha kutaka kummeza. Yanga wameshtuka! Wanadai hawezi kuwa mkubwa kuliko klabu. Lakini hapo hapo wanaikumbuka mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC). Wanaiona chungu. Hawana Balama. Wanawweza kumkosa Mo Banka. Morrison naye ndiye huyo. Pia hawana uhakika wa Papy Tshishimbi ambaye naye anatajwa kuwatikisa vigogo, ili asaini upya. Kwa namna ninavyowajua mashabiki wa Yanga walivyo. Morrison aombee Kariakoo Derby, iishe kwa Yanga kutupwa nje ya michuano, vinginevyo atajuta kuwafahamu. Kama Yanga itapasuka kwa mnyama. Baadhi wanaweza kulegeza nati na kuamini wamefungwa kwa vile BM33 hayupo.

Hata yeye anajionea fahari, lakini Yanga ikishinda bila ya yeye kuwapo uwanjani. Itakuwa mateso kwake. Kadhalika hata kama ataamua kuondoka Jangwani na pengine kutua Msimbazi. Asitarajie mafanikio, labda awe na miujiza kuliko aliyoifanya Yanga. Hatacheza kwa amani.

Badiliko alilokumbana nalo Morrison Yanga katika hizi sarakasi zake zinakumbusha zile nyodo anazodaiwa kuzifanya Said Sued ‘Scud’ miaka ya mwanzoni mwa 1990. Scud sio kama alikana mkataba ama la, lakini wachezaji wenzake wanadai baada ya kuifunga Simba mara mbili msimu wa 1991 alivimba kichwa. Hakuwa na uzoefu wowote wa mechi kubwa, kipindi hicho akiwa na umri usiozidi miaka 25 akitokea timu ya Kurugenzi Kigoma, jamaa aliwalaza njaa Simba.

Wapo wanaodai kidume hicho kilichokuwa na mwili wa kushiba alikuwa akiugusa mguu wake, huku akiusifia kwa kumzima Simba. Kilichompata kila mmoja anakijua. Alipotea na kusahaulika kwenye soka kwa sasa inaelezwa anaendelea na maisha yake kule kwao Kigoma. Nini kilichomkuta hata akashindwa kusikika tena kwenye soka. Jibu analo mwenyewe kidume hicho kilichokuwa kinapenda kunyoa panki kama lile la Willy Mtendawema ama marehemu David Mjanja. Ngoja tuone kama kweli kesi ya Morrison kwa Yanga itaendelea baada ya mechi ya Julai 12. Yetu macho tu!