Madrid yaichapa Barca nyumbani, Messi atoka kapa

BARCELONA, HISPANIA. Real Madrid imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Barcelona kwenye mechi ya Ligi Kuu Hispania ikiwa ni miongoni mwa mchezo mikubwa inayofutiliwa na wapenzi wa soka duniani.

Bao la kwanza la Madrid liliwekwa wavuni na Federico Valverde dakika ya tano kabla ya Ansu Fati kusawazisha akimalizia pasi iliyopigwa na Jordi Arba dakika ya nane na kufanya hadi mapumziko kwenda zikiwa sare.

Timu zote zilitawala mpira na kucheza soka la kushambulia hadi Madrid walipopata penalti baada ya marejeo ya VAR iliyoonyesha Clement Lenglet alimchezea vibaya nahodha Sergio Ramos kwa kumvuta jezi na alipiga mwenyewe na kufunga.

Bao la kuwalaza na viatu Barca iliyokuwa inaongozwa na Lionel Messi liliwekwa wavuni kiufundi na Luca Modric aliyeingia dakika ya 69 akimpiga chenga golikipa Neto kisha kupiga shuti lilioenda wavuni.

Real Madrid imepanda kileleni kwa msimamo wa ikifikisha alama 13 baada ya mechi sita na Barcelona imeporomoka hadi nafasi ya 12 ikiwa na alama saba akishinda mechi mbili, droo moja na kufungwa miwili.

Lakini pia mchezo huo wa El Clasico, umekuwa wa kwanza kuchezwa bila ya mashabiki tangu marufuku ya mshabiki kutoingia viwanjani ilipochukua nafasi kutokana na janga la virusi vya corona na mechi hiyo ya El Clasico imekuwa ya sita mfululizo kwa Messi kushindwa kutupia bao.