Madrid wanusa ubingwa Hispania

Friday July 3 2020

 

MADRID, HISPANIA. JANA kulikuwa na michezo mitatu ndani ya Ligi Kuu nchini Hispania, ambapo Real Madrid ilizidi kufifisha matumaini ya Barcelona kutwaa ubingwa msimu huu, baada ya kufanikiwa kushinda dhidi ya Getafe bao 1-0.

Katika mchezo huo ulioonekana kuwa mgumu na kusababisha kipindi cha kwanza kuisha kwa sare ya bila bila, Madrid ilipata bao mnamo dakika ya 79 kupitia mkwaju wa penati uliopigwa na Kapteni wao Sergio Ramos.

Mpaka filimbi ya mwisho inapulizwa kuashiria kuisha kwa mchezo huo, Madrid walitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0.

Matokeo hayo yana wafanya Madrid kufikisha jumla ya alama 74 na kuacha nafasi ya alama nne dhidi ya mpinzani wake Barca ambaye anashika nafasi ya pili akiwa na alama 70, huku wote wakiwa wamecheza mechi 33.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane alizungumzia mchezo huo na kusema kuwa bado mapambano yanaendelea,

" Tumeshinda lakini siwezi kusema chochote, bado tuna michezo mitano inayofuata, kwangu ni kama hatujashinda kitu, ingawa zilikuwa ni pointi tatu muhimu, bado tunahitaji kuendelea kupambana zaidi, tuna furaha juu ya umoja wetu katika timu, na hilo ndio jambo zuri kwetu"alisema

Advertisement

" Ingawa tumepata ushindi kiugumu sana, lakini huu ndio mpira, inawezekana mechi ijayo dhidi ya Espanyol tukapata ugumu kama huu tena" aliongeza.

Michezo mengine ilikuwa ni kati ya;

Eibar wanaoshika nafasi ya 16 akiwa na alama 35, waliwaalika  Osasuna wanaoshika  nafasi ya 11 na pointi 44, mchezo ambao uliisha kwa wenyeji Eibar kukubali kichapo cha mabao 2-0.

Real Sociedad wakiwa nyumbani waka waalika  RCD Espanyol katika mchezo uliotamatika kwa Sociedad kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Baada ya mchezo huo Sociedad amepanda hadi nafasi ya saba akiwa na alama 50 baada ya kucheza mechi 33.

Leo Julai kutakuwa na mchezo mmoja kati ya Atletico Madrid dhidi ya Real Mallorca ambao utapigwa saa  3:00 usiku. Atletico ana jumla ya pointi 59, baada ya kucheza mechi 33 na anashika nafasi ya tatu.

Huku Mallorca wao wanashika nafasi ya 18, baada ya kucheza mechi 33 na kukusanya alama 29.

Advertisement