Madadi: Matajiri wanaingilia makocha

Muktasari:

Hata hivyo, Madadi aliyeiongoza Simba kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) mwaka 1992 pale Zanzibar alipambana na kupinga kitendo hicho.


MKURUGENZI wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi ametoa ushuhuda wa baadhi ya makocha wanavyoingiliwa wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Amesema baadhi ya viongozi na wafadhili wa klabu kubwa wamekuwa wakiingilia kazi za makocha ikiwemo kupanga vikosi kwenye baadhi ya mechi hasa za watani wa jadi.

Kauli hiyo ya Madadi imetokana na kitendo kilichofanywa mwaka 1992 na kufichua kwamba, suala la makocha kupangiwa vikosi halikuanza leo.

Hata hivyo, Madadi aliyeiongoza Simba kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) mwaka 1992 pale Zanzibar alipambana na kupinga kitendo hicho.

“Wafadhili wote wa Simba wakiongozwa na Azam (Dewji) walitaka kunipangia kikosi, ilifika wakati nilibaki na Juma Salum (aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, sasa marehemu). Kulikuwa na tuhuma ya baadhi ya wachezaji wa Simba kuhongwa na mfadhili wa Yanga wakati huo, Abbas Gulamali (naye ni marehemu),” alisema Madadi.

“Hivyo wafadhili wa Simba hawakutaka niwapange wachezaji kama wanane hivi wa kikosi cha kwanza, lakini nilipambana nao hadi dakika ya mwisho na nikawachezesha wachezaji hao.”

Mchezo huo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar ulimalizika kwa ushindi kwa Simba wa penalti 5-4.

Awali timu hizo zilikuwa zimetoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na vitimbi vingi uliomaliza dakika 120 bila ya bingwa kupatikana.

Kesho Mwanaspoti litaanza kuchapisha mfululizo wa simulizi za Madadi kuhusiana na mchezo huo ulivyozua balaa na mambo mengine mengi kumhusu. Ungana naye kuanzia kesho Ijumaa.