Mada Maugo apata udhamini mnono

Muktasari:

Maugo alisema, udhamini wa PAEG umekuja wakati muafaka na kusisitiza kuwa umemuongezea chachu ya kupambana na kufanya vizuri ndani na nje ya nchi.

Bondia Mada Maugo amepata udhamini mnono wa Kampuni ya Pan African Entertainment Group (PAEG) inayofanya bahati nasibu ya Hela Bet.
Maugo ambaye anajiandaa kuzichapa na Twaha Kiduku, Machi 2 mkoani Morogoro atakuwa balozi wa Hela Bet ambayo itamdhamini kwa makubaliano maalumu.
Akizungumza na gazeti hili, Maugo alisema udhamini wa PAEG umekuja wakati muafaka na kusisitiza kuwa umemuongezea chachu ya kupambana na kufanya vizuri ndani na nje ya nchi.
Ofisa Mtendaji mkuu (CEO) wa PAEG, Barney Barrow amesema wameamua kumdhamini Maugo kutokana na uwezo wake kwenye ngumi.
"Maugo atakuwa balozi wa PAEG kupitia chapa ya Hela Bet, ambayo ni mchezo wa bahati nasibu tunayokuja kuianzisha nchini hivi karibuni," amesema Barrow.
Alisema watafanya kazi na Maugo kwa mkataba mnono ingawa hakuutaja ni kiasi gani, lakini akasisitiza utamnufaisha bondia huyo lakini pia kampuni yao.
"Kwenye mapambano yake atavaa nembo ya Hela Bet, lakini pia mbali na mambo mengine, tutampa vifaa vya mazoezi na mashindano kwa kipindi chote cha mkataba," alisema Brrow.